Featured Kitaifa

TUPANUE WIGO KUTAMBUA MATATIZO YANAYOSABABISHA AFYA DUNI YA AKILI- SERIKALI

Written by mzalendoeditor

 

 Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii Baraka Makona,akizungumza wakati akifungua kikao kazi cha Wataalam wa Ustawi wa Jamii wanaotoa huduma ya afya ya akili na msaada wa kisaikolojia kilichofanyika jijiji Arusha.

Sehemu ya washiriki wakimsikiliza Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii Baraka Makona (hayupo pichani) wakati akifungua kikao kazi cha Wataalam wa Ustawi wa Jamii wanaotoa huduma ya afya ya akili na msaada wa kisaikolojia kilichofanyika jijiji Arusha.

Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii Baraka Makona,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua kikao kazi cha Wataalam wa Ustawi wa Jamii wanaotoa huduma ya afya ya akili na msaada wa kisaikolojia kilichofanyika jijiji Arusha.

Na WMJJWM, Arusha

Wataalam wa Ustawi wa Jamii wanaotoa huduma ya afya ya akili na msaada wa kisaikolojia wameaswa kuongeza wigo wa huduma hiyo ili kuisaidia jamii na matatizo ya Afya ya akili na saikolojia.

Hayo yamesemwa na Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii Baraka Makona kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju katika kikao cha kikosi kazi kilichofanyika Septemba18, 2023 jijiji Arusha.

Makona amebainisha kuwa lengo la kikao hicho ni kuimarisha uratibu na ushirikiano katika kutekeleza utoaji wa huduma ya afya ya akili na msaada wa kisaikolojia nchini.

Aidha Kamishna Msaidizi Makona ameainisha miongoni mwa sababu zinazopelekea afya duni ya akili kwa mujibu wa Ripoti ya Afya ya akili iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) Mwaka 2017 kuwa ni mabadiliko ya mara kwa mara ya kijamii, kutengwa na kijamii, Mtindo wa maisha usiozingatia kanuni za kiafya, uhatarishi wa vitendo vya ukatili na ukiukwaji wa Haki za Binadamu.

“Sababu hizi nilizozianisha zinaonesha kuwa kuna uhusiano mkubwa wa kushamiri kwa vitendo vya ukatili katika jamii na tatizo la afya duni ya akili kwa ujumla, tuchukue hatua sisi wataalam tuisaidie jamii” alisema Makona.

Ameeleza pia jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali kwa lengo la kutokomeza vitendo vya ukatili nchini na kuimarisha afya ya akili, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA), Utekelezaji wa Sera ya mwaka 2007 na Sera nyingine nyingi zenye lengo la kuimarisha afya ya akili.

Vile vile amewataka wajumbe katika kikao hicho kuhakikisha utekelezaji wa huduma hiyo unajumuisha maeneo yote hasa katika makundi maalum, maeneo ya kazi na jamii kwa ujumla, kwani kwa sasa kumekuwa na wimbi kubwa la wananchi kujidhuru, kujiua na kuuwana na mengi yao yakisababishwa na changamoto ya afya ya akili.

“Aidha kuhakikisha uwepo wa mpango wa awali wa kuandaa mkakati wa miaka mitano wa utoaji wa huduma ya msaada wa kisaikolojia nchini” ameeleza Makona.

Ameiasa jamii kuwa changamoto ya matatizo ya kisaikolojia na afya ya akili isichukuliwe kuwa ni ugonjwa ambao suluhu yake ni hospitali tu, bali ni lazima kutanua wigo wa kutambua matatizo mengineyo yanayoigusa jamii na kupelekea tatizo hilo na namna ya utatuzi sahihi, ikiwa ni pamoja na kuwahusisha viongozi wa dini katika utatuzi wa changamoto hizo.

About the author

mzalendoeditor