Featured Kitaifa

WAANDISHI WA HABARI WAPONGEZWA KUELIMISHA WANANCHI WAKATI WA SENSA

Written by mzalendoeditor

Na Mwandishi Wetu – Njombe

Waandishi wa habari nchini wamepongezwa kwa kazi kubwa ya kuelimisha na kuhamasisha wananchi wakati wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi Mwaka 2022, wametakiwa kuendeleza kazi hiyo kwa kutoa habari sahihi za matokeo ya Sensa yanayoendelea kutolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Hayo yameelezwa leo Septemba 18, 2023 na Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Mhe. Anne Makinda mjini Njombe wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa waandishi wa habari wa mikoa ya Njombe na Ruvuma ili waweze kuandika na kuripoti kwa ufasaha matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi yanayoendelea kutolewa na NBS.

“Wakati wa Sensa ya mwaka 2022 mlifanya kazi nzuri ya kuelimisha wananchi, sasa matokeo yanaendelea kutolewa, tunaamini kwamba mtatumia mafunzo haya kufanya kazi ya kutafsiri matokeo yanayotolewa ili wananchi wayatumie kufanya maamuzi”, alisisitiza Mhe. Makinda.

“Ukitoa habari yako iaminike na kukubadilika na Wananchi kwa namna ulivyozingatia taaluma ya Uandishi wa habari”, alisisitiza Mhe. Makinda

Akieleza zaidi Mhe. Makinda amesema kuwa nchi yoyote ikitaka kuendelea lazima itumie takwimu sahihi na kwa sasa Tanzania inazalisha takwimu ambazo Waandishi wa Habari wanaowajibu wa kuwaelimisha wananchi ili wazitumie.

Mafunzo kwa Waandishi wa Habari 70 kutoka mikoa ya Njombe na Ruvuma yanafanyika kwa siku mbili mjini Njombe kuanzia Septemba 18 – 19, 2023.

About the author

mzalendoeditor