Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Angela Muhozya akifanya maombi ya kumshukuru Mungu kwa kufanikisha matibabu ya mgonjwa kutoka nchini Malawi Anna Kamwaza wakati wa kumpa ruhusa ya kurejea nchini kwake baada ya afya yake kuimarika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akisikiliza mapigo ya moyo ya mgonjwa kutoka nchini Malawi Anna Kamwaza aliyelazwa katika Taasisi hiyo kwa ajili ya kupatiwa matibabu na kuruhusiwa wiki hii baada ya hali yake kuimarika.
Baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wanaofanya kazi katika kliniki ya VIP wakimpatia vipeperushi vinavyoelezea huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo mgonjwa kutoka nchini Malawi Anna Kamwaza baada ya kufanyiwa upasuaji wa tundu dogo na kuwekewa kifaa cha kuusaidia moyo kusukuma damu vizuri (Cardiac Resynchronization Therapy Device – CRTD) wakati wa kuruhusiwa mapema wiki hii baada ya hali yake kuimarika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimuaga mgonjwa kutoka nchini Malawi Anna Kamwaza baada ya kufanyiwa upasuaji wa tundu dogo na kuwekewa kifaa cha kuusaidia moyo kusukuma damu vizuri (Cardiac Resynchronization Therapy Device – CRTD) wakati wa kuruhusiwa mapema wiki hii baada ya hali yake kuimarika.
Picha na: JKCI
…………………..
Wagonjwa kutoka nje ya nchi wafurahia huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kuwafanya kujisikia kama wapo katika nchi zao.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hii kwa nyakati tofauti wagonjwa hao walisema kuwa wataalamu wa afya wa JKCI ni wakarimu na wanatoa huduma kwa upendo huku wakiwajulia hali zao mara kwa mara kuhakikisha kuwa wapo sawa.
Wagonjwa hao pia wameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwekeza vifaa vya kisasa vya matibabu ya moyo katika Taasisi hiyo vinavyotumika kuuchunguza moyo vizuri na vingine kutumika katika kutoa huduma za matibabu ya kibingwa ikiwemo upasuaji wa moyo.
Anna Kamwaza mgonjwa kutoka nchini Malawi alisema uwepo wake katika Taasisi hiyo kwa kipindi cha wiki mbili akipatiwa matibabu kutokana na tatizo lake la moyo kutanuka na uwezo wa moyo kusukuma damu kuwa chini kumemkutanisha na familia ya watanzania hivyo kujisikia kama yupo nyumbani.
Anna alisema alinza kusumbuliwa na tatizo la sukari lililopelekea kupata shida ya moyo na kutibiwa katika hospitali mbalimbali nchini Malawi bila ya mafanikio hadi alipopata taarifa za JKCI kupitia kambi maalum ya matibabu iliyofanyika nchini Malawi naye kuwa mmoja wa watu waliopatiwa huduma katika kambi hiyo na kupewa rufaa kufika JKCI kwa ajili ya matibabu zaidi.
“Nilivyosikia kuhusu kambi maalum ya matibabu ya moyo iliyokuwa ikifanywa na madaktari wa JKCI nilifika kwa ajili ya kuangalia tatizo langu kama litapatiwa ufumbuzi, sikujali foleni iliyokuwepo na hata nilivyoambiwa nirudi kesho yake nilifanya hivyo maana nilikua natafuta ufumbuzi wa tatizo langu”,
“Nilipewa rufaa kufika JKCI kwa ajili ya matibabu zaidi, kwakweli hapa JKCI nimekuta huduma nzuri sana sikutegemea kama hapa Afrika tunaweza kuwa na hospitali nzuri hivi, pongezi nyingi ziende kwa Serikali ya Tanzania na uongozi wa JKCI, naahidi kuwa balozi mzuri nchini Malawi kuwaelezea wenzangu wenye shida ya moyo kufika hapa kwani huduma za kibingwa zinapatikana JKCI”, alisema Anna
Kwa upande wake Daktari aliyemfanyia upasuaji mgonjwa huyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Yona Gandye alisema walimpokea mgonjwa huyo uwezo wa moyo wake kusukuma damu ukiwa na asilimia 38 hivyo kumuwekea kifaa maalum cha kuusaidia moyo kusukuma damu vizuri (Cardiac Resynchronization Therapy Device – CRTD) na kuweka sawa msukumo wa damu.
Dkt. Gandye alisema upande mmoja wa moyo wa Anna ulikuwa ukichelewa kupata msisimko unaosaidia kusukuma damu hivyo kusababisha moyo kufanya kazi kwa kiwango kikubwa na kumsababishia mgonjwa kuhisi kuchoka mara kwa mara, kushindwa kutembea umbali mrefu au kufanya kazi ngumu.
“Baada ya kumchunguza mgonjwa tuliona upande mmoja wa moyo haupati msisimko unaopelekea kusukuma damu inavyotakiwa hivyo kumuwekea kifaa maalum cha CRTD kusawazisha pande zote mbili za moyo ziwe na msisimko sawa wa kuwezesha damu kusukumwa vizuri”, alisema Dkt. Gandye.
Naye mzazi ambaye mtoto wake amefanyiwa upasuaji wa moyo JKCI kutoka nchini Kongo Mwamini Rebeka alisema mtoto wake amezaliwa na magonjwa ya moyo lakini hakuweza kutambua mapema kutokana na kutokuwepo na huduma za matibabu hayo eneo analoishi.
Mwamini alisema kwa kipindi cha miaka tisa amekuwa akimpeleka mtoto wake hospitali mbalimbali hadi kufikia mwaka huu alipogundulika kuwa na tatizo la moyo na kuanza kutafuta matibabu nchini Rwanda na baadaye kushauriwa kufika Tanzania Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.
“Namshukuru Mungu mtoto wangu kafanyiwa upasuaji wa moyo wa kuziba matundu kwenye moyo hapa JKCI, awali nilishauriwa niende nchini India au Ufaransa ndio nitapata matibabu baadaye ndugu zangu watanzania wakaniambia hakuna haja yakwenda nchi za mbali kwani matibabu hayo pia yanapatikana hapa JKCI”, alisema Mwamini.
Akizungumzia wagonjwa wanaotoka nje ya nchi Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema wagonjwa kutoka nchi za Afrika sasa hawana haja ya kwenda nchi za mbali kwa ajili ya matibabu ya kibingwa ya moyo kwani matibabu hayo yanapatikana JKCI.
Dkt. Kisenge alisema sasa wagonjwa wengi wa moyo waliopo nchi zinazoizunguka Tanzania wanafika JKCI kupatiwa matibabu na wengi wao wamekuwa mabalozi wazuri kutokana na kuridhika kwa huduma wanazozipata JKCI.
“JKCI imewekeza katika kutoa huduma bora kwa wateja, wagonjwa wetu wengi kutoka nje ya nchi wanatupongeza kwa kazi nzuri tunayoifanya kuanzi eneo la kupokea wagonjwa na maeneo mengine yote ambayo mgonjwa anapitia. Wagojwa kutoka nje ya nchi msisite kufika JKCI kwa ajili ya kupata huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwani tupo kwaajili yenu”, alisema Dkt. Kisenge
JKCI imekuwa ikipokea wagonjwa kutoka nje ya nchi zikiwemo nchi za Malawi, Visiwa vya Comoro, Kongo, Kenya, Uganda, Msumbiji, Burundi, Somalia, Rwanda, Zambia, Ethiopia na wengine kutoka nje ya Afrika zikiwemo nchi za Armenia, China, India, Norway, Marekani na Uingereza.