Featured Kitaifa

WAZIRI MAKAMBA AKABIDHIWA RASMI OFISI

Written by mzalendoeditor

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akikabidhiwa nyaraka mbalimbali na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.  

………

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) amekabidhiwa ofisi rasmi na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mhe. Waziri Makamba amemshukuru Dkt. Tax kwa ushirikiano aliompatia wakati wote tangu yalipofanyika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri mwishoni mwa mwezi Agosti 2023.

“Tangu Mheshimiwa Rais alipofanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri umekuwa ukinipatia ushirikiano wakati wote, nakushukuru sana, pia nakutakia heri katika majukumu yako mapya” amesema Waziri Makamba

Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Tax amesema alipohudumu katika Wizara alipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa menejimenti na watumishi wa Wizara na kumhakikishia Mhe. Waziri Makamba kuwa ana watumishi wachapakazi

“Wakati wa utumishi wangu hapa wizarani, nilipata ushirikiano mkubwa, hivyo napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru sana menejimenti na watumishi wote wa wizara kwa ushirikiano walionipa,” alisema Dkt. Tax

Amesema jukumu lililo mbele ya Wizara hii ni kutekeleza maono ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa vitendo kwa kutafuta fursa mbalimbali za kukuza uchumi na kuendeleza Diplomasia ya Uchumi

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Tax pia amemtakia utendaji kazi mwema Waziri Makamba na kuwashukuru Naibu Waziri Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) Katibu Mkuu Mkuu wa Wizara, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Naibu Katibu Mkuu, Menejimenti na watumishi wa Wizara.

Makabidhiano hayo yalihudhuriwa pia na wajumbe wa menejimenti na baadhi ya watumishi wa wizara.

About the author

mzalendoeditor