Featured Kitaifa

PROF. MAKULILO: AKILI BANDIA, CHANGAMOTO MPYA KATIKA MACHAPISHO YA KITAALUMA

Written by mzalendoeditor
Maendeleo ya Teknolojia yamekuja na manufaa makubwa lakini papo hapo katika uandishi wa kazi za kitaaluma yameleta changamoto nyingi ikiwemo utengenezaji wa machapisho kupitia akili bandia kunakofanywa na baadhi ya watu wasiowaaminifu.
 
Hayo yamesemwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) anayesimamia Teknolojia za Kujifunzia na Huduma za Mikoa, Prof. Alex Makulilo, wakati akizindua mafunzo ya uhariri kwa wahariri wakuu wa majarida ya kitaaluma kwa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yanayofanyika katika chuo cha Uongozi cha Mwl. Julius Nyerere kilichopo Kibaha mkoani Pwani.
 
Prof. Makulilo amesema, kwa sasa teknolojia imerahisisha sana upatikanaji wa machapisho ya kujisomea kupitia mitandao mbalimbali na pia kurahisisha ufanyikaji wa tafiti mbalimbali. Hata hivyo, kuna watu ambao si waamnifu wanaweza kutumia akili bandia kutengeneza machapisho na kuwafanya waonekane wana uwezo mkubwa wa kufanya utafiti na kutoa machapisho mengi kwa mwaka lakini kiuhalisia hawajafanya utafiti bali ni akili bandia ndio iliyofanya kazi ya kuzalisha machapisho hayo.
 
“Akili bandia ina uwezo wa kuzalisha andiko au hata kitabu, hii imelazimisha baadhi ya taasisi za elimu ya juu kutoa angalizo kwa wanataaluma na wanafunzi kukiri kama kazi wanazotoa ni za kwao au wamezipata kupitia akili bandia. Hili hufanyika kupitia mfumo maalumu unaojulikana kama Plagerism check. Hivyo, katika mfunzo haya moja ya mjadala uwe ni namna ambavyo ninyi kama wahariri mnavyoweza kukabiliana na tatizo hili linalotokana na maendeleo ya teknolojia.” Amesema Prof. Makulilo.
 
Aidha, ameogeza kuwa, kinachofanya nchi nyingi za Afrika kuwa nyuma katika tafiti na kutoa machapisho yaliyo bora ni ufinyu wa bajeti za utafiti. Serikali nyingi barani Afrika zinatenga bajeti ndogo au kutotenga kabisa bajeti za utafiti jambo linalofanya watafiti kujigharamia wenyewe kwa fedha kidogo walizonazo na hivyo kutofikiwa kwa ubora wa utafiti na machapisho yatokanayo na utafiti huo.
 
Akizungumzia warsha hiyo, Mkurugenzi wa Utafiti, Machapisho na Ugunduzi wa chuo hiki, Dr. Harrieth Mtae, amesema kwa sasa kuna uhitaji mkubwa wa majarida kwa ajili ya kupokea machapisho kutoka kwa wanataaluma na watafiti. Hii ni kutokana na serikali ya Tanzania kuhamasisha ufanyaji wa utafiti vyuoni ikijumuisha wahadhiri na wanafunzi. Hata hivyo, pamoja na uhitaji huo kuwa mkubwa bado utokaji wa machapisho hayo umekuwa ukisuasua.
 
“Haya mafunzo ni katika kuboresha majarida yaliyopo chuoni. Chuo hiki kina majarida saba lakini utokaji wake umekuwa siyo katika mpango wa vipindi au muda wa utokaji unaotakiwa. Hivyo mafunzo haya yametukutanisha wahariri wote ili kuona wapi panatukwamisha ikizingatiwa uhitaji wa watu kutoa machapisho ni mkubwa sana.” Amesema Dkt. Mtae.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shahada za Juu za Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambaye pia ni Mhariri Mkuu wa jarida la Huria, Prof. Magreth Bushesha, amesema mafunzo hayo ni muhimu sana kwao kwa sababu yanakwenda kutatua changamoto ambazo wamekuwa wakikutana nazo katika kuhudumia majarida yaliyopo.
 
“Kwa mfano, jarida la Huria linakubalika sana hapa Tanzania na duniani kwa jumla, tunapata mawasilisho mengi ya makala kwa ajili ya kuyachapisha. Hapa tutajadili changamoto zilizopo ili jarida liweze kukua zaidi. Hawa wawezeshaji wamekuja kutukumbusha mambo muhimu tunayopaswa kuyafahamu, ukumbusho huu utatufanya kuamka na kutuwezesha kudhibiti changamoto zote ili majarida yetu yote ikiwemo la Huria yaweze kufika katika viwango vya juu zaidi kidunia.” Amesema Prof. Bushesha.
 
Naye mwezeshaji wa mafunzo hayo Prof. Lazarus Ndiku Makewa, amesema wanatoa mafunzo hayo ili kuweza kuyafanya majarida yote kuwa hai na kazi za kitaaluma ziweze kuchapishwa kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
 
Mafunzo haya ya uhariri kwa Wahariri wa majarida ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), yaliyoandaliwa na kurugenzi ya Utafiti, Machapisho na Ugunduzi, yamefanyika kwa siku mbili kuanzia Septemba 06 mpaka Septemba 07, 2023 katika Chuo cha Uongozi cha Mwl. Julius Nyerere kilichopo Pwani Kibaha. Wahariri wamekumbushwa kufanya kazi kwa weledi ili kutoa machapisho bora kwa wakati kwa lengo la kuendelea kuzalisha maarifa, ujuzi, gunduzi na bunifu katika jamii ya Watanzania, Afrika na duaniani kwa jumla.

About the author

mzalendoeditor