NAIBU Katibu Mkuu,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Dk. Charles Msonde,akizungumza wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo waratibu wa Mpango wa shule salama na wasimamizi wa usalama wa jamii wa mikoa na halmashauri yaliyofanyika leo Septemba 8,2023 jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
NAIBU Katibu Mkuu,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Dk. Charles Msonde amewataka wazazi, walezi na jamii kutoacha mzigo wa malezi ya watoto kwa walimu pekee badala yake washirikiane nao katika kuwalinda ili wanapopata changamoto wawe wazi kwao.
Dk. Msonde ameyasema hayo leo Septemba 8,2023 jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo waratibu wa Mpango wa shule salama na wasimamizi wa usalama wa jamii wa mikoa na halmashauri.
“Malezi na ulinzi wa mtoto ni jukumu letu sote hivyo wazazi,walezi na jamii ishirikiane vyema na shule wasiwaachie tu walimu kwani mtoto anaweza kupata changamoto nyumbani, kwenye jamii ama shuleni hivyo ni muhimu kuwalinda kwa pamoja.
“Mwalimu anakuwa wa kwanza kabisa kumuona mtoto anapokuwa na changamoto kwa sababu watoto wengi wanakuwa wawazi na huru kuwaelezea walimu wao changamoto wanazozipitia hata kuliko ilivyo kwa wazazi wao”amesema Dk. Msonde
Aidha amesema kuwa katika kutekeleza Mpango wa shule salama ni lazima kila shule kuwa na mwalimu Mnasihi ambaye watoto watamtumia kutoa kero ambazo wanakabiliwa nazo wakati wanapokuwa shule, nyumbani au njiani wakati wa kwenda au kurudi nyumbani.
“Lazima shule kuwa na walimu wanasihi ambao watachaguliwa na wanafunzi wenyewe ambao watoto wa shule watawatumia kueleza changamoto zao ili kulinda usalama wa mtoto”alisema
Amesema katika mradi wa kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) serikali imewekeza kiasi cha Sh.trilioni 1.2 na mradi huo umekuwa ukisaidia katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika shule za sekondari.
“Kwa sasa wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza imeongezeka na mradi wa SEQUIP umelenga kujenga shule 1,026 na katika shule hizo 26 ni shule maalum kwa ajili ya wasichana na kila mkoa utajengwa shule moja”amesema
Hata hivyo, amewataka wakurugenzi katika halmashauri zote nchini kuhakikisha miradi yote inatekeleza kama mwongozo ulivyoelekeza na ikamilike kwa muda uliopangwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi anayesimamia Idara ya Elimu kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Vincent Kayombo, amesema maafisa 630, wanashiriki mafunzo hayo.
“Ni imani yangu kubwa kuona matokeo ya mafunzo haya yanakwenda kuleta tija katika shule na jamii kwa ujumla kila mmoja akatambue umuhimu wa malezi na ulinzi wa usalama wa watoto”amefafanua