Featured Kitaifa

KATAMBI: SERIKALI IMEWEKA MFUMO WA UFUATILIAJI NA TATHMINI YA PROGRAMU ZA VIJANA

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi  akijibu swali bungeni, jijini Dodoma leo tarehe 4 Septemba, 2023.

………

Na: Mwandishi Wetu, DODOMA

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi  amesema serikali imeweka mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ya miradi na programu za vijana ili kupima matokeo ya utekelezaji sambamba na kuleta tija kwa Taifa.

Mhe. Patrobas Katambi ameyasema hayo bungeni 4 Septemba, 2023 alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti maalum (CCM), Mhe. Ng’wasi Damas Kamani ambaye amehoji serikali inatumia mfumo gani kuhakiki ubora na matokeo chanya ya programu zinazotekelezwa na vijana.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Katambi amesema serikali ilitoa mwongozo wa kitaifa wa ufuatiliaji na tathmini wa miradi na programu za maendeleo ambapo Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikifanya ufuatliaji wa utekelezaji wa programu kila robo mwaka.

Pia, amesema serikali imepanga kufanya tathmini mahususi (Tracer Study) ya mafunzo yanayotolewa kupitia programu za kuwezesha vijana ili kubaini mafanikio yaliyopatikana katika kuwezesha vijana kujiajiri au kuajiriwa.

About the author

mzalendoeditor