Featured Kitaifa

DKT. BILAL AITAKA TAASISI YA NELSON MANDELA KUZIDI KUNG’ARA KATIKA TAFITI

Written by mzalendoeditor

 

Makamu wa Rais Mstaafu  na Aliyekuwa Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia Dkt. Mohamed Gharib Bilal akiongea wakati wa  hafla ya kuwasimika  Mkuu wa taasisi  Bw. Omari Issa na  Makamu Mkuu wa taasisi , Profesa Maulilio Kipanyula.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia, anayeshughulikia masuala ya Sayansi  Profesa James Mdoe akizungumza na Watumishi wa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia pamoja na wageni waalikwa wakati wa Hafla ya Kuwasimika Mkuu wa Taasisi na Makamu Mkuu  wa taasisi.

Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia  Bw. Omari Issa akitoa neno la shukrani wakati wa hafla ya kusimika viongozi wa Taasisi hiyo Agosti 30,2023.

Makamu wa Rais Mstaafu  na Aliyekuwa Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia Dkt. Mohamed Gharib Bilal  (kulia) akimsimika Mkuu wa Taasisi  Bw. Omari Issa (Katikati) Agosti 30,2023, Kushtoto ni Mkuu wa Ndaki Sayansi ya Viumbe Hai na Bailojia  Professa Ernest Mbega.

Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia  Bw. Omari Issa (Kushoto) akimsimika Makamu Mkuu wa Taasisi Prof. Maulilio Kipanyula (katikati)  , kulia ni Mkurugenzi wa Taaluma Dkt. Efraim Kosia.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia, anayeshughulikia masuala ya Sayansi  Profesa James Mdoe (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na menejimenti ya Taasisi  wakati wa Hafla ya Kuwasimika Mkuu wa Taasisi na Makamu Mkuu  wa taasisi Agosti 30,2023.

Na  Mwandishi Wetu, Arusha

Makamu wa Rais Mstaafu  na Aliyekuwa Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia Dkt. Mohamed Gharib Bilal ameitaka Taasisi hiyo kuzidi kung’ara katika masuala ya tafiti na bunifu  kwa maendeleo ya nchi na Afrika kwa ujumla.

Dkt. Bilal ameyasema hayo  Agosti 30, 2023  wakati wa hafla ya kumsimika Mkuu wa taasisi hiyo mpya Bw. Omari Issa sanjari na kumsimika Makamu Mkuu wa taasisi , Profesa Maulilio Kipanyula.

“Ninahamu ya kuona taasisi hii inapiga hatua zaidi na najua mwenzangu Bw. Omari Issa ataiweka taasisi hii katika anga za juu zaidi” alisema Dkt. Bilal

 Aliongeza kuwa  taasisi ya Nelson Mandela  ni imara na  ya kipekee  nchini  hivyo anatamani kuiona  ikipaa  zaidi katika anga za juu katika tafiti , bunifu na teknolojia huku  akiwapongeza watumishi wa taasisi hiyo kwa kuhakikisha jina la NM-AIST linapaa zaidi.

Naye Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia, anayeshughulikia masuala ya Sayansi  Profesa James Mdoe  ameeleza kuwa wizara ina matarajio makubwa kupitia uongozi huo mpya ikiwemo kuongeza mchango wa sayansi na teknolojia katika kuchagiza maendeleo ya nchi.

“Mmemsikia Mkuu wa chuo anataka ongezeko la wanawake chuoni hapa ili kupata wanataaluma wengi zaidi katika sayansi na teknolojia “Alisema Naibu Katibu Mkuu  Professa James Mdoe

Professa Mdoe anaeleza kuwa  kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEETProject) Wizara kupitia Vyuo Vikuu  inatarajia kuanzisha kozi maalum ili kuwasaidia wanawake wasiofikia ufaulu waweze kupata ufaulu na kuruhusu kujiunga na vyuo vikuu  ili kuongeza msukumo kwa wanawake na wasichana  kujiunga na vyuo vya Sayansi na Teknolojia.

Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi  Bw. Omari Issa anaeleza  kuwa uongozi wa Dk. Bilal umefanikiwa katika mambo mbalimbali ikiwemo ongezeko la udahili wa wanafunzi kutoka wanafunzi 80  hadi kufikia wanafunzi 1,468 na ujenzi wa Bweni linaloendelea kujengwa ambalo linauwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 500 na vyumba maalum kwa ajili ya   wanafunzi wakike wanaonyonyesha na wajawazito.

“Naomba nisisitiza udahili wa wanafunzi wa kike  lazima uongezeke zaidi kwani wanawake wanaweza zaidi katika nyanja za kila aina hivyo katika kipindi cha uongozi wangu udahili wa wanawake uzingatiwe”. Bw. Omari Issa

Hafla hiyo ya kusimikwa kwa Wakuu wa Taasisi umehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mwakilisha wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha ambaye ni Afisa Elimu Taaluma Mkoa Bw. Emmanuel Mahundo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia upande wa Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe na  Mwenyekitiwa Baraza la Chuo na Mkuu wa Chuo cha Dodoma Professa Lughano Kusiluka.

About the author

mzalendoeditor