Featured Kitaifa

SERIKALI YAISHUKURU CHINA KWA UFADHILI WANAFUNZI 30

Written by mzalendoeditor

 

SERIKALI  ya Tanzania imeishukuru Serikali ya China kwa kutoa fursa na kufadhili wanafunzi 30 kutoka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kwenda kusoma programu ya uhandisi nchini humo kupitia Kampuni ya Group Six International & Sino Tan Industrial Park.

Akizungumza jijini Dar es Salaam mara baada ya kukabidhi bendera ya Tanzania kwa wanafunzi hao Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa hati ya makubaliano ambayo ilisainiwa mapema mwezi Desemba 2022 kuhusu ushirikiano wa kutoa mafunzo kwa pamoja kati ya DIT na Chuo cha Chongqing Vocational Institute of Enginnering cha nchini China.

Amesema China ni nchi iliyoendelea kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia na hivyo kama nchi tunahitaji kujifunza kutoka kwao ili kuweza kuwa na ujuzi na kutoa mchango katika nchi yetu.

“Tunahitaji sana kujifunza kutoka nchini China, kuna kitabu kimoja kitakatifu kinasema tafuteni elimu hata China, kwa hiyo twende china tujifunze sayansi teknolojia na mafunzo ya amali,” amesema Prof. Mkenda

Akizungumzia program ambayo wanafunzi hao wanakwenda kusoma Waziri Mkenda amesema ni ya miaka miwili ambayo itawawezesha kupata diploma ya Tasisi hiyo lakini pia miaka miwili hiyo itahesabika kama sehemu ya miaka minne ya Programu ambayo wanasoma hapa nchini.

“Kati ya miaka minne ya masomo Wanafunzi hawa tayari wameshasoma mwaka mmoja hapa DIT na kufanya mafunzo kwa vitendo kwenye Kampuni ya Group Six International & Sino Tan Industrial Park kwa miezi miwili. Hivyo watatumia miaka miwili nchini China na watarejea kumalizia mwaka mmoja hapa DIT na kupata shahada katika eneo hilo,” amesema Waziri Mkenda

Na kuongeza “Programu hiyo ni muhimu kwa kuwa inaendana na maono ya Rais Samia ambayo aliwaahidi watanzania baada ya kuingia madarakani na kulihutubia Bunge Aprili 22, 2021 kuwa anataka kuona elimu inayotolewa inakuwa elimu ujuzi ili wanaomaliza wawe wanaajirika kirahisi au kujiajiri.

Waziri Mkenda amemshukuru Mwenyekiti wa Group six International & Sino Tan Industrial Park Janson Huang, Bodi ya DIT na Menejimenti kwa juhudi za kuhakikisha wanafunzi hao wanakwenda China kusoma huku akiwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili watakaporejea wawe bora na wenye ujuzi wa kuweza kujiajiri ama kuajirika na kuchangia maendeleo ya nchi.

Wakati huohuo Mkenda amesema nia ni kuhakikisha idadi ya wanafunzi wanaoenda katika programmu hiyo inaongezeka na kuhimiza wakufunzi pia kuenda kusoma huko.

Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam Mhandisi Prof. Preksedis Ndomba amesema Wanafunzi hao kwenda China ni kutoka na makubaliano ambayo DIT imeingia na Chuo cha Chongqing Vocational Institute of Enginnering cha nchini humo kushirikana kwenye mafunzo na kwamba wanafunzi waliochaguliwa ni wale waliofanya vizuri katika masomo yao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kampuni ya Group Six International & Sino Tan Industrial Park Mr Janson Huanga amesema wanafunzi hao wanaokwenda China watasoma kwa miaka miwili na wakihitimu watatunukiwa diploma ya Taasisi hiyo.

About the author

mzalendoeditor