Featured Kitaifa

KATAMBI: TUNAENDELEA KUTOA ELIMU YA KANUNI ZA MAFAO

Written by mzalendoeditor

 

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi  akijibu swali bungeni jijini Dodoma leo Agosti 29, 2023.

Na Mwandishi Wetu, DODOMA

SERIKALI imeendelea kutoa elimu ya kanuni mpya ya mafao ya pensheni (kikokotoo) na hadi Juni 30, mwaka huu wanachama wa mifuko ya pensheni 131,497 na waajiri 5,580 wamefikiwa na elimu hiyo.

Adha, Elimu hiyo imetolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi  amebainisha hayo bungeni Agosti 29, 2023 alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Moshi Mjini (CCM), Mhe. Priscus Tarimo aliyetaka kujua mpango wa serikali kuhusu malalamiko ya wastaafu juu ya kikokotoo kinachotumika kupiga mahesabu na kulipa mafao.

Mhe. Katambi amesema mpango wa serikali ni kuendelea kuwaelimisha wananchi hususani waajiri na wanachama wa mifuko hiyo wakiwamo wastaafu kuhusu faida ya kanuni hizo.

Amesema kwasasa kwenye mkupuo wa malipo wanufaika asilimia 81 ya wanachama wote na asilimia 19 mafao yao ya kila mwezi yameongezeka kupitia kanuni hizo.

“Katika malipo yale ya kila mwezi kulikuwa kuna asilimia 50 walikuwa wanalipwa lakini sasa wamefikia asilimia 67 ya malipo, haya maboresho yametokana na utafiti uliofanyika na utaratibu wa kuunganisha mifuko ya pensheni imeleta tija kubwa,” amesema

About the author

mzalendoeditor