MCHEZAJI Max Mpia Nzengeli akiwa na wenzake wakishangilia bao baada ya kufunga dakika y 7 mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali uliochezwa uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam Yanga washinda mabao 5-1
Na.Alex Sonna-Mzalendo blog
MABINGWA wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania bara Timu ya Yanga SC imetinga hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika baada ya kupata ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Asas Djibouti mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali uliochezwa uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.
Wakicheza mbele ya mashabiki wao huku wakiita siku ya Max Day kwa mtindo wake wa kuchomekea Yanga SC walianza kupata bao dakika ya 7 likifungwa na Max Mpia Nzengeli kwa kichwa akimalizia pasi ya Jesus Moloko.
Licha ya kupata bao Yanga SC waliendelea kucheza mpira safi na wa kuvutia huku Shangwe za Mashabiki zikitawala uwanja wa Azam Complex mnamo dakika ya 45 Mshambuliaji kutoka Ghana Hafiz Konkini akimalizia Mpira wa Stephane Aziz Ki.
Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga SC kufanya mabadiliko kwa kuwatoa Jesus Moloko,Aziz Ki,Mkunde,Bacca na kuwaingiza Nkane,Mauya,Pacome Zouzou,Mzize na kuendelea kuishambulia
Kiungo Mshambuliaji na Mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Ivory Coast, Pacome Zouzou alifanya balaa katika lango la wapinzani kwa kuwapiga chenga mabeki na Kipa na kufunga bao la Kimataifa mnamo dakika ya 55.
Mshambuliaji Kinda Clement Mzize alipigilia chuma cha nne katika dakika ya 69 akifunga bao safi kwa kichwa akimalizia Krosi ya Nickson Kibabage.
Asas Djibouti walipata bao dakika ya 85 likifungwa kwa Mkwaju wa Penalti na Tito Mayor baada ya Kiungo Mkabaji Gift Mauya kucheza rafu ndani ya 18 na mwamuzi kuamua kuwa Penalti.
Max Mpia Nzengeli alirudi tena kwenye kamba mnamo dakika ya 90 + 1 akifunga bao la tano baada ya kumalizia Mpira wa Clement Mzize.
Kwa ushindi Yanga SC wameiondosha Asas Djibouti jumla ya mabao 7-1 baada ya mchezo wa kwanza kushinda kwa mabao 2-0 na sasa rasmi itaanza ugenini dhidi ya El Merreikh ya Sudan ambao wamechagua kutumia uwanja wa Huye uliopo nchini Rwanda.