Featured Kitaifa

MAANDALIZI YA TAMASHA LA KITAIFA LA UTAMADUNI NJOMBE YAMEKAMILIKA

Written by mzalendoeditor

Na Eleuteri Mangi, WUSM, Njombe

Maandalizi ya Tamasha la Pili la Kitaifa la Utamaduni yamekamilika na mikoa zaidi ya 26 inatarajiwa kushiriki tamasha hilo ambalo litafanyika kwa siku tatu kuanzia Agosti 25 – 27, 2023 katika viwanja vya stendi kuu ya zamani mkoani Njombe.

Akiongea mara baada ya kumaliza mbio za polepole (jogging) Agosti 24, 2023, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni, Dkt. Resani Mnata amesema maandalizi yamekamilika tayari kwa tamasha la pili na shamrashamra zimeanza kwa jogging ikihusisha makundi mbalimbali ikiwemo vikundi vya watumishi wa umma, jogging vya Njombe, polisi, timu ya veteran pamoja na wanafunzi kutoka shule mbalimbali mjini humo.

“Wananchi wanakaribishwa kutumia fursa ya huduma za afya itakayotolewa wakati wote wa tamasha ili waweze kupima bure wa afya zao kwa magonjwa yasioambukiza, tutakuwa pia na michezo mbalimbali ikiwemo mechi baina ya washabiki wa timu za Simba na Yanga mkoani humo, wananchi wote mnakaribishwa” amesema Dkt. Resani Mnata.

Tamasha hilo litashirikisha mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani na kutoa fursa kwa Watanzania kusherehekea utajiri wa urithi wa Utamaduni na kuwahamasisha wananchi wapende kuhifadhi, kulinda, kuendeleza mila na desturi ambazo ndio msingi wa maadili na utambulisho wa Taifa letu.

Tamasha hili litapambwa na shughuli mbalimbali zitakazofanywa na Serikali na wananchi. Shughuli hizo ni Bonaza la Michezo litakalowahusisha Machifu, Viongozi wa dini, Madiwani, viongozi wengine wa Kijamii na wananchi na kutakuwa na usiku wa Filamu za Harakati za Ukombozi.

About the author

mzalendoeditor