Featured Kitaifa

TAKUKURU YAZUIA  NONDO ZISIZO NA VIWANGO UJENZI WA BARABARA YA MZUNGUKO DODOMA

Written by mzalendoeditor

MKUU  wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),Mkoa wa Dodoma,Bw John Joseph,akizungumza na waandishi wa habari kuhusu  utendaji kazi katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Aprili hadi Juni mwaka huu leo Agosti 23,2023 jijini Dodoma.

Na.Alex Sonna-DODOMA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Dodoma,imefanikiwa kuzuia matumizi ya nondo tani 120 zisizokuwa na ubora ambazo zilipangwa kutumika katika ujenzi wa barabara ya mzunguko nje (Ring-road) yenye kilomita 52.3 ya Nala-Veyula na Ihumwa- Bandari
Kavu,iliopo jijini Dodoma.

Hayo yameelezwa leo Agosti 23,2023 jijini Dodoma na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma,Bw John Joseph, wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu  utendaji kazi katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Aprili hadi Juni mwaka huu.

Bw.Joseph amesema  TAKUKURU ilibaini Mkandarasi alipanga kutumia tani 120 za nondo ambazo ziko chini ya kiwango zenye thamani ya sh.milioni 204 ambapo kamazingetumika mradi ungetekelezwa chini ya kiwango .

“Baada ya njama hizo kubainika TAKUKURU ilichukua hatua za udhibiti ikiwa ni pamoja na kuziondoa tani zote za nondo ambazo zilikuwa eneo la ujenzi na Mkandarasi mshauri alishauriwa kuongeza umakini,”amesema Bw.Joseph

Hata hivyo amesema TAKUKURU Dodoma,imefanikiwa kudhibiti wizi wa sh milion 3.9
kutoka kwa mtumishi wa halmashauri ya wilaya ya Chemba ambazo ni za
wanufaika wa Mfuko wa TASAF wa kijiji cha Mlongia kilichopo wilaya
humo,kwa ajili ya kukatiwa Bima ya Afya ilioboreshwa (CHF).

“Baada ya TAKUKURU kupata taarifa na kuingilia kati mtumishi huyo amerejesha fedha hizo na tayari zimewasilishwa katika mfuko wa bima ya afya kwa ajili ya kuwakatia bima ya afya wanufaika 130 wa mfuko wa TASAF,”ameeleza

Aidha amesema kuwa wamefanya utekelezaji wa miradi 64 ya miradi ya maendeleo
yenye thamani ya sh billioni 12.7,ambayo ni ya Elimu,Afya,Ujenzi,Maji,
na Mifugo, ambapo katika ufuatiliaji huo wameweza kuokoa kiasi cha sh
Milion 41.2 ambazo zilikuwa katika hatari ya kufanyiwa ubadhilifu.

About the author

mzalendoeditor