Featured Kitaifa

MBUNGE LUCY MAYENGA AKABIDHI MAJIKO 760 KWA MAMA LISHE MKOA WA SHINYANGA

Written by mzalendoeditor
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga Mhe.  Lucy Mayenga ametoa msaada wa majiko ya gesi 760  yenye thamani ya shilingi Milioni 45.6 kwa wajasiriamali mbalimbali wakiwemo mama lishe mkoani Shinyanga ikiwa ni sehemu ya  kampeni yake aliyoianzisha ya matumizi ya nishati sahihi ya kupikia na utunzaji wa mazingira.

 

 
Kampeni hiyo awamu ya kwanza ameihitimisha leo Agosti 22,2023  kwa kugawa majiko 165 yenye thamani ya shilingi milioni 9.9 kwa mama lishe katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga. 
 
Akizungumza wakati hafla hiyo ya ugawaji majiko ya gesi, Mhe. Mayenga amesema alimua kuchagua wajasiriamali kada ya wanawake hususan mama lishe kwani ndiyo wamekuwa wakikabiliana na changamoto nyingi za kimaisha hivyo kumuwezesha mwanamke ni kuiwezesha jamiii nzima.
 
“Mwezi uliopita niligawa majiko kwa mama lishe wilayani Kahama, jana pia nimekabidhi majiko ya gesi 160 yenye thamani ya shilingi milioni 9.6 kwa akina mama lishe katika wilaya ya Kishapu kwenye ukumbi wa SHIRECU uliopo wilayani kishapu na leo nimegawa majiko 165 yenye thamani ya shilingi milioni 9.9 kwa mama lishe katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, jumla ya majiko niliyogawa mpaka sasa ni 760. Naahidi kuendelea na kampeni hiyo ya kwa awamu ya pili lengo likiwa ni kuwafikia wanawake wajasiriamali 1500 mkoa wa Shinyanga”,amesema Mhe. Mayenga.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mayenga amewaomba wanawake kuiunga mkono serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu kwani imekuwa na dhamira njema katika kumaliza changamoto zinazowakabili wanawake ikiwemo miradi ya maji yenye dhamira ya kumtua mama ndoo kichwani na matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kumtua mama kuni kichwani.

 
Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake (UWT) mkoa wa Shinyanga, Grace Bizuru amewataka wanawake kupendana huku akimshukuru Mhe. Lucy Mayenga kwa kuzunguka mkoa mzima na kutoa majiko kwa wanawake wajasiriamali kwani yatawarahisishia katika shughuli zao ikiwa ni pamoja na utunzaji mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
 
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wawanawake wa CCM (UWT) wilayani Kishapu Rahel madundo amesema msaada huo ni muhimu sana kwani utaondoa tatizo la vikongwe kuuawa kwa imani za kishirikina kwa kuonekana wana macho mekundu kwa sababu ya matumizi ya nishati isiyo safi kwa kupikia lakini pia msaada huo utarahisisha shughuli za upishi na biashara kwa mama lishe.
 
 
Nao baadhi ya wajasirimali waliopata msaada huo wamemshukuru mbunge huyo kwa kampeni hiyo huku wakiahidi kutunza mazingira kwa kutokata miti ovyo kwa ajili ya kuni na mkaa kwani kwa sasa wana nishati sahihi ya kupikia.
 

Kampeni ya matumizi ya nishati sahihi ya kupikia awamu ya kwanza ilianzishwa na mbunge huyo mwezi Julai 2023 na kutelekezwa katika wilaya zote za mkoa wa Shinyanga kwa ugawaji wa majiko ya gesi kwa wajasiriamali.

Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga Mhe.  Lucy Mayenga (katikati) akikabidhi jiko la gesi kwa mmoja wa wajasiriamali

 

 

About the author

mzalendoeditor