Featured Kitaifa

WODI YA MAMA NA MTOTO YA KISASA KUJENGWA NEWALA KUBORESHA HUDUMA

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nambunga alipopewa fursa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kuzungumza na wananchi hao.

Wananchi wa Newala wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) alipopewa fursa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kuzungumza nao walipokusanyika eneo la Stendi ya Mabasi ya Newala.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Newala alipotembelea hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Newala kukagua ujenzi wa miundombinu ya afya.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akikagua miundombinu iliyojengwa na Serikali katika hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Newala.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala alipopewa fursa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kuzungumza na wananchi hao mara baada ya kukagua ujenzi wa jengo la utawala katika halmashauri hiyo.

Na: James Mwanamyoto (OR-TAMISEMI)

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi amesema Serikali ya Awamu ya Sita itajenga wodi ya mama na mtoto ya kisasa katika Hospitali ya Wilaya ya Newala ili kuboresha utoaji wa huduma ya afya ya uzazi.

Mhe. Ndejembi amesema hayo akiwa katika Wilaya ya Newala, mara baada ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kumpatia fursa ya kuzungumza na wananchi wa eneo hilo. 

Mhe. Ndejembi amefafanua kuwa, wodi hiyo ikikamilika itawawezesha wananchi kupata huduma za kisasa badala ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma katika hospitali ya rufaa ya mkoa.

Sanjari na hilo, Mhe. Ndejembi amesema Serikali imetoa shilingi milioni 600 katika jimbo la Newala Mjini kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya viwili kwa gharama ya milioni 250 kwa kila kituo, ikiwa ni pamoja na zahanati moja itakayogharimu shilingi milioni 100.

Ameongeza kuwa, Serikali imetoa gari mbili za wagonjwa (Ambulance) pamoja na gari lingine atakalokuwa akilitumia Mganga Mkuu wa Wilaya kutembelea zahanati na vituo vya afya ili kuhimiza utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Aidha, Mhe. Ndejembi ameanisha kuwa Halmashauri hiyo ilikuwa ikikabiliwa na changamoto ya baadhi ya kata kukosa shule ya Sekondari lakini kiasi zaidi ya bilioni 209 kilichotolewa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kujenga shule za sekondari nchini kimeiwezesha Halmashauri hiyo kupata shule katika kata zake.

“Hapa Newala mmepata milioni 560 ya kujenga shule mpya ya sekondari ambayo ujenzi wake unaendelea na katika mwaka wa fedha uliopita mlipata shilingi milioni 470 za ujenzi wa shule na kwasasa imebaki kata moja tu kupata shule lakini Serikali inatafuta fedha ili kujenga shule katika kata hiyo,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amehitimisha ziara ya kikazi ya siku mbili katika Wilaya za Tandahimba na Newala iliyolenga kukagua ujenzi wa miundombinu ya afya na elimu ambayo inajengwa ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

About the author

mzalendoeditor