Featured Kitaifa

WMA YAONYA WAUZAJI MITUGI YA GESI INAYOTUMIKA MAJUMBANI 

Written by mzalendoeditor

 

AFISA  Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA) Bi. Stella Kahwa, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Agosti 15,2023 jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya wakala huo na mwelekeo wa mwaka wa fedha 2023/24.

Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya habari-MAELEZO Bw.Gerson Msigwa,akizungumza mara baada ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA) Bi. Stella Kahwa,kutoa taarifa  kuhusu utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya wakala huo na mwelekeo wa mwaka wa fedha 2023/24.

Na.Alex Sonna-DODOMA

AFISA  Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA) Bi. Stella Kahwa,amewataka  wauzaji wa mitungi ya gesi inayotumika majumbani kwa ajili ya kupikia kuwa na mizani itakayotumika kupima ujazo halisi ili kuondokana na malalamiko ya wananchi kutapeliwa.

Hayo ameyasema leo Agosti 15,2023 jijini Dodoma wakati  akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya wakala huo na mwelekeo wa mwaka wa fedha 2023/24.

Bi.Kahwa, amesema kuwa kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kutapeliwa kiasi kinachouzwa kwenye mitungi ya gesi kuwa tofauti na ujazo halisi uliondikwa.

“Kuna watu wanalalamika kuwa wananunua mtungi wa gesi lakini wanautumia kwa muda wa siku mbili hali ambayo ni kinyume na sheria za wakala huu lazima wauzaji wote wawe na mizani kwa ajili ya kupima ujazo wa gesi lakini pia mizani kwa ajili ya kupima uzito wa mtungi wenyewe ili mteja ajue ni kilo ngapi kanunua”amesema Bi.Kahwa

Hata hivyo amesema kuwa  muuzaji kupima mtungi wa gesi kabla hajamuuzia mteja ni suala la lazima siyo hiyari na mteja anapaswa kuhakikisha kuwa bidhaa alionunua inaujazo halisi uliondakiwa na siyo vinginevyo.

Amesema wakala huo unalo jukumu la kusimamia kiasi cha gesi inayoingia nchini kwa meli zitokazo nje ya nchi ili kujua kiasi cha gesi hiyo (LPG) iliyoagizwa na wafanyabiashara ili kujiridhisha kuwa wanunuzi wa bidhaa hiyo wanapata kiasi sahihi kulingana na thamani ya fedha iliyolipwa.

Pia amesema kuwa pamoja kuhakiki kiasi cha gesi toka nje ya nchi pia wanafanya ukaguzi na uhakiki wa mitungi ya gesi ya ujazo tofauti tofauti ili kuhakikisha kuwa wanunuzi wa gesi hiyo ya kupikia majumbani wanapata kiasi sahihi kulingana na thamani ya fedha waliyolipa,

Katika sekta ya maji alisema Wakala huo kwa sasa unafanya uhakiki wa Dira zote za maji zinazotumiwa na Mamlaka za maji kwa wateja wao.

“Uhakiki unafanywa kwa dira zote mpya na zile ambazo tayari zipo katika matumizi ili kuhakikisha Mamlaka za maji zinapata tozo sahihi kwa maji yaliyotumiwa na mteja na mteja nae analipa gharama sahihi kulingana na maji aliyoyatumia”amesema

About the author

mzalendoeditor