Featured Kitaifa

MIRADI YA TEHAMA IWASILISHWE e-GA

Written by mzalendoeditor

Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), imezitaka taasisi za umma kuhakikisha kuwa miradi na mifumo yote ya TEHAMA inayotekelezwa ndani ya taasisi zao inawasilishwa e-GA wakati wa hatua ya mipango ili kuiwezesha Mamlaka kupitia na kutoa ushauri wa kitaalamu kabla ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Kauli hiyo imetolewa leo na Meneja wa Usimamizi wa Udhibiti na Viwango vya Serikali Mtandao Bi. Sultana Seiff, wakati wa kufunga mafunzo ya siku mbili kwa Maafisa TEHAMA na Rasilimali watu kutoka katika taasisi mbalimbali za umma zilizo katika Sekta ya uchukuzi yaliyofanyika mkoani Morogoro kuanzia Agosti 09, mwaka huu.
Alibainisha kuwa, agizo hilo ni utekelezaji wa matakwa ya kifungu Na. 24 cha Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019 pamoja na Kanuni Na.27 ya Kanuni za Jumla za Serikali Mtandao za mwaka 2020.
“Taasisi zote za umma zinapaswa kuwasilisha taarifa kamili na sahihi za miradi na mifumo yote ya TEHAMA kupitia Tovuti ya Huduma za TEHAMA Serikalini ijulikanayo kama ‘Government ICT Service Portal (GISP)’ ili e-GA ifanye mapitio ya miradi hiyo na kutoa ushauri wa kitaalam pamoja na kibali” Alisema Bi. Sultana.
Aidha, alifafanua kuwa pamoja na uwepo wa sheria hiyo, Mamlaka imeandaa viwango na miongozo ya Serikali Mtandao ambayo taasisi zote za umma zinapaswa kuzingatia katika usimamizi na utekelezaji wa miradi, mifumo na miundombinu ya TEHAMA ili kuhakikisha kuwa jitihada hizo zinakua ni salama, sahihi, bora, endelevu, na zenye kuzingatia thamani halisi ya pesa.
Lengo la Mamlaka ya Serikali Mtandao ni kuhakikisha taasisi za umma zinatumia TEHAMA katika utendaji kazi wake na utoaji wa huduma kwa wananchi ili huduma hizo zipatikane kwa wananchi wote kwa wakati mahali walipo na kwa gharama nafuu, alisema.
Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA Wizara ya Ujenzi na uchukuzi katika Sekta ya Uchukuzi Bw. Leonard Lwiza, alisema ufanisi wa utendaji kazi katika sekta ya Uchukuzi unategemea ujenzi na uwepo wa mifumo salama na imara ya TEHAMA hivyo ni muhimu mifumo hiyo izingatie Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao.
Aidha, aliwataka Maafisa TEHAMA walioshiriki mafunzo hayo, kuwa mawakala wazuri kwa kuhakikisha kuwa, miradi na mifumo yote ya TEHAMA katika taasisi zao inazingatia sheria, kanuni, viwango na miongozo ya Serikali Mtandao.
Naye Afisa Rasilimali watu kutoka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Bw. Bakari Mbaga aliishukuru e-GA kwa kuandaa mafunzo hayo kwani yamewajengea uwezo kuhusu Sheria, viwango na miongozo ya Serikali Mtandao na umuhimu wake katika kuhakikisha taasisi za umma zinatumia vema TEHAMA ili kuimarisha jitihada za Serikali Mtandao.

About the author

mzalendoeditor