Featured Kitaifa

SEKTA YA KILIMO INA MCHANGO MKUBWA UKUAJI WA UCHUMI – MHE. KATAMBI

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Agosti 8, 2023 akizungumza na wananchi waliohudhuria katika viwanja vya Nzuguni Dodoma katika kilele cha sikukuu ya wakulima (Nanenane) kanda ya kati.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Agosti 8, 2023 akiwasili katika viwanja vya Nzuguni Dodoma katika kilele cha sikukuu ya wakulima (Nanenane) kanda ya kati.

Na: Mwandishi Wetu – Dodoma

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amesema sekta ya kilimo ina mchango mkubwa kwenye maendeleo ya ukuaji wa uchumi nchini.

Mhe. Katambi amebainisha hayo Agosti 8, 2023 wakati wa kilele cha sherehe na siku kuu ya Wakulima (nane nane) kanda ya kati katika viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma.

Amesema kuwa zaidi ya asilimia 80 ya watanzania wanategemea kilimo, uvuvi na ufugaji kwa ustawi wa maisha yao.

Aidha, Mhe. Katambi amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka dhamira ya dhati kuhakikisha inaimarisha kilimo cha umwagiliaji ili kupunguza utegemezi wa mvua na kuimarisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo na mifugo kupitia mfumo wa ruzuku.

Kwa upande mwengine, Naibu Waziri Katambi amezitaka halmashauri na mashirika ya umma na binafsi yanayoshughulika na kilimo kuweka mipango ya kuwasajili wakulima ili wanufaike na fursa ya kutumia ruzuku za serikali.

Pia, ametoa wito kwa taasisi za kifedha kukopesha vijana, wanawake na Watu wenye Ulemavu wanaojishughulisha na kilimo, ufugaji na uvuvi ili waweze kupata mitaji ya kuendeleza shughuli hizo.

Maonesho na Sherehe za Nanenane Mwaka 2023 yalikuwa na kaulimbiu isemayo “VIJANA NA WANAWAKE NI MSINGI IMARA YA MSINGI IMARA WA MIFUMO ENDELEVU YA CHAKULA”.

About the author

mzalendoeditor