Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo (MOI) Prof. Abel Makubi ,akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 3,2023 jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya MOI ndani ya miaka miwili ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na mipango ya mwaka wa fedha 2023/2024.
Sehemu ya Waandishi wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo (MOI) Prof. Abel Makubi (hayupo pichani) akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya MOI ndani ya miaka miwili ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na mipango ya mwaka wa fedha 2023/2024.
Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya habari-MAELEZO Bw.Gerson Msigwa,akiipongeza MOI mara baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo (MOI) Prof. Abel Makubi kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya MOI ndani ya miaka miwili ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na mipango ya mwaka wa fedha 2023/2024.
Na.Alex Sonna-DODOMA
KATIKA mwaka wa Fedha 2023/24 Serikali imetenga jumla ya Shilingi Bilioni 55.9 ili kuboresha huduma za tiba na shughuli za uendeshaji ikiwemo kuongeza ubora wa huduma zote ndani ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo (MOI) ili kukidhi matarajio ya wananchi na kufikia viwango vya kimataifa kwa utoaji wa huduma za tiba.
Hayo yamesemwa leo Agosti 3,2023 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo (MOI) Prof. Abel Makubi wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya MOI ndani ya miaka miwili ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na mipango ya mwaka wa fedha 2023/2024.
Prof.Makubi amesema MOI wanatarajia Kuanzisha huduma mpya tatu za kibingwa kibobezi ambazo bado zinasababisha rufaa nje nchi (Tiba ya baadhi ya Kiharusi kupitia Angio-suite, Tiba ya baadhi ya vifafa kupitia upasuaji na upasuaji wa kiuno kwa njia ya matundu (Hip arthroscopy)
”Tunaanza na Ujenzi mpya wa miundombinu ikiwemo jengo jipya la wagonjwa wa nje (OPD) ambalo litakuwa na vyumba 30 vya kliniki vya kisasa tofauti na vyumba 7 vilivyopo sasa, ujenzi wa hospitali ya kisasa ya utengamao, mazoezi ya viungo na upasuaji wa mifupa (Rehabilitation and Spine centre) katika kiwanja cha MOI chenye ukubwa wa hekari 10 kilichopo Mbweni Mpiji Mbweni jijini Dar es salaam, kuhakikisha vifaa tiba vinapatikana muda wote ambapo zimetengwa Shilingi bilioni 2 kwa mwaka huu.”amesema Prof.Makubi
Amesema kuwa ili Kupunguza gaharama za upasuaji kwa kununua vifaa moja kwa moja kutoka viwandani
”Tumeendelea kuwapa mafunzo wataalamu wetu ili kuwaongezea ujuzi ambapo wataalamu 10 wanapelekwa kwenye mafunzo kupitia mfuko wa mafunzo wa Mama Samia na kuendelea kujengea uwezo watumishi wa Hospitali zingine za Kanda na Mikoa ili kupunguza mrundikano wa wagonjwa MOI na kutoa nafuu ya gharama kwa Wananchi.”amesema
Aidha amesema kuwa wataendelea Kutoa elimu kwa kushirikiana na mamlaka nyingine ili kupunguza ajali za barabarani na kukabiliana na majeruhi kwa haraka.
Amesema kuwa wataendelea Kuimarisha uwajibikaji na usimamizi kwa viongozi na watumishi ndani ya taasisi.
”Tutaendelea kushirikiana na MUHAS, MNH, JKCI na Taasisi zingine katika kutoa Mafunzo na Tafiti katika eneo la Tiba ya Mifupa na Ubongo.”amesema
Hata hivyo amesema kuwa MOI imeendelea kuwajengea uwezo wataalamu wa hospitali kubwa za Bugando, Mbeya, KCMC, Benjamin Mkapa, Hospitali ya rufaa ya Nkinga-Tabora na Mnazi mmoja Zanzibar ili waweze kutoa baadhi ya huduma za kibingwa na kibobezi zinazotolewa MOI.
”Katika Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar zaidi ya wagonjwa 30 wamefanyiwa upasuaji wa kubadilishiwa Nyonga na magoti na Madaktari Bingwa wa MOI ambapo zaidi ya wagonjwa 100 walihudumiwa katika kliniki za wagonjwa wa nje.”amesema Prof.Makubi
Aidha amesema kuwa serikali imeokoa shilingi bilioni 195.2 ambazo zitatumika kwa shughuli nyingine za maendeleo ya nchi na kupunguza rufaa.
“Upasuaji mpya wa Kibobezi au zilizofufulia na kuimarishwa Katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya awamu ya Sita, MOI imeanzisha huduma mpya, kufufua na kuziimarisha kwa kufanywa na Watalaamu Mabingwa wa hapa nchini baada ya Serikali kutoa fedha zaidi ya TZS Bil 4.5 kwa ajili ya vifaa,
Huduma ya kuondoa uvimbe kwenye sakafu ya ubongo kupitia tundu la pua (transsphenoidal hypophysectomy): Wagonjwa 31 wameshafanyiwa upasuaji,”amesema
Pia amesema kuwa Gharama za upasuaji huo hapa nchini ni Tsh milioni 8 16 na nje ya nchi ni zaidi ya Tsh milioni 40.
Taasisi imeanzisha huduma ya matibabu ya maumivu sugu ya mgongo bila ya upasuaji, toka kuanza kwa huduma hii mei 2023 tayari wagonjwa 97 wamepata huduma hii,Gharama za upasuaji huu hapa nchini ni Tsh milioni 1 na nje ya nchi ni zaidi ya milioni 9.
Aidha amesema katika kipindi tajwa, Taasisi imeanzisha huduma mpya ya utengenezaji wa mkono wa umeme ambapo tayari wagonjwa 5 wameshahudumiwa.
Prof.Makubi amesema kuwa Gharama zake ndani ya nchi ni Tsh milioni 15 na nje ya nchi ni milioni 30 mpaka 60 Serikali kuhudumia Wananchi Wasiokuwa na Uwezo Serikiali kupitia MOI ilitoa misahama yenye gharama ya TZS 6.5 billion/miaka miwili kwa Wananchi wasio na uwezo na ambao pia hawakuwa na Bima za afya ili kuwawezesha kupata Huduma za Uchunguzi, madawa na upasuaji.
Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya habari-MAELEZO Bw.Gerson Msigwa amewahimiza watanzania kujenga utamaduni wa kutibiwa hospitalini kabla ya kwenda kwenye tiba mbadala ili uwekezaji uliofanywa na serikali uwe na tija kwao.
”Wananchi jengeni utamaduni wa kwenda kupata matibabu hospitalini, Serikali yetu imefanya mapinduzi makubwa katika kuimarisha huduma kwenye hospitali yetu ya MOI na zingine nchini, wananchi zitumieni, msikae na wagonjwa nyumbani na msiwapeleke wagonjwa tiba mbadala (waganga wa kienyeji), msisubiri wagonjwa wazidiwe na kuwapeleka wagonjwa hospitali wakiwa wameshafika katika hali mbaya.”amesema Bw.Msigwa
Aidha amesema kuwa serikali inaendelea kuboresha huduma za matibabu katika hospitali zote kuanzia ngazi ya Wilaya katika kutoa huduma za kibingwa na kibobezi, vile vile Serikali imeanza kujenga vituo vya afya kuanzia ngazi ya Kata.