Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya mauaji ya kinyama ya Mzee Minza Madaha, aliyekuwa mkaazi wa Mtaa wa Ng’wanakiboro, Kata ya Bunamhala, Tarafa ya Ntuzu Wilaya ya Bariadi mkoa wa Simiyu mnamo tarehe 31 Julai, 2023.
Mama huyo wa miaka 85 aliyekutwa amefariki nyumbani kwake imeripotiwa amegundulika alikatwa na kitu chenye ncha kali maeneo ya usoni na sababu inayotajwa ni ushirikina. Tukio hilo linafanyika wakati Serikali pamoja na Wadau wanaendelea na jitihada za kutokomeza ukatili dhidi ya wazee na kulinda usalama wao.
Kutokana na juhudi hizo, matukio ya mauaji dhidi ya Wazee yalikuwa yametoweka ambapo Takwimu zinaonesha mwaka 2021 hakukuwa na tukio lolote la mauaji. Aidha, kwa miaka ya nyuma matukio hayo yanaonesha kupungua mathalani; matukio 203 (2017), 93(2018), 74(2019), 54(2020) na 0(2021). Hata hivyo, matukio haya yalionekana kuongezeka tena hadi 130 mwaka 2022 hivyo bado tunahitaji ushirikiano na jamii ili kutokomeza matukio haya ili yasitokee na yawe historia nchini.
Tunaendelea kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Simiyu na Vyombo vya Dola kuhakikisha wahusika wa mauaji hayo wanakamatwa na kushugulikiwa kwa mujibu wa Sheria.
Natumia nafasi hii kukemea vikali na kutoa onyo kwa wahusika wa mauaji hayo na wote wanaopanga kufanya uhalifu wa aina hiyo dhidi ya Wazee kwa kisingizio cha ushirikina. Aidha natoa rai kwa wanajamii kuchukua jukumu la kuwalinda na kuwatunza Wazee na kuhakikisha wanakuwa salama katika jamii na kuepukana na vitendo vya ukatili dhidi yao. Vilevile, nawakumbusha wananchi kushirikiana na Serikali kwa kutoa taarifa za viashiria vyovyote vya ukatili kabla madhara hayajatokea.
Dorothy Gwajima (Mb)
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,
WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM