Featured Kitaifa

WAFANYAKAZI WA HOTELINI WAHIMIZWA KUJIUNGA NA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII

Written by mzalendoeditor

 

Na Mwandishi Wetu, Arusha

Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imetoa wito kwa wafanyakazi wa hotelini kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii ili kujiwekea akiba itakayowasaidia kwenye maisha yao.

Ofisa kutoka Idara ya Hifadhi ya Jamii wa Ofisi hiyo, Charles Liganya ametoa rai hiyo Julai 28, 2023 jijini Arusha alipokuwa akitoa elimu kwa wafanyakazi wa hotelini wanaopewa mafunzo ya kukuza ujuzi kwa uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi.

Liganya amesema wafanyakazi hao wanapaswa kujiunga na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili waweze kunifaika na Mafao yatolewayo na mfuko huo.

Pia amewahakikishia kuwa sekta ya hifadhi ya jamii kwa ujumla inasimamiwa vema na Ofisi ya Waziri Mkuu (Idara ya Hifadhi ya Jamii) na kama kuna changamoto ambayo haijatatuliwa na mfuko wawasilishe kwenye Idara hiyo ili kushughulikiwa.

Naye, Mkurugenzi Msaidizi wa Ukuzaji Ujuzi kutoka Ofisi hiyo, Robert Masingiri, amesema suala la bima ya afya na pensheni ni kwa wafanyakazi hao ili kuwa na uhakika wa matibabu na maisha yao.
Awali, Meneja Huduma kwa Wanachama kutoka NSSF, Robert Kadege, amesema mfuko una utaratibu wa kisheria wa kufuatilia michango ya mwanachama kwa mwaajiri wake ikiwamo kuwafikisha mahakamani ili kunusuru michango ya wafanyakazi ambao haijawasilishwa NSSF.

 

About the author

mzalendoeditor