Featured Kitaifa

DK. NDUMBARO ATAKA HOSPITALI YA WILAYA SONGEA IKAMILIKE KWA WAKATI, UBORA

Written by mzalendoeditor

 

Mbunge wa Songea Mjini ambaye pia ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dk. Damas Ndumbaro amewataka wataalam wa Halmashauri ya Songea pamoja na mkandarasi anayejenga hospitali ya Wilaya ya Songea kuongeza kasi na ubora wa ujenzi wa hospitali hiyo.

Mhe.Ndumbaro ametoa rai hiyo wakati wa ziara yake pamoja na Kamati ya Siasa ya Mkoa na Wilaya kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo inayojengwa katika Mtaa wa Sanangura, Kata ya Tanga wilayani Songea.

“Wananchi hawa wamenipa ridhaa ya kuwatumikia na ni jukumu langu kuhakikisha natafuta fedha kwa ajili ya maendeleo yao na nimekuja leo kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwemo huu wa hospitali.

Kwa wataalamu wetu, rai yangu, muhakikishe mnasimamia ujenzi huu unakamilika kwa wakati na kwa ubora tuliokubaliana ili wananchi hawa waanze kupata huduma haraka kama tulivyo waahidi,” amesema Mhe.Ndumbaro huku akiwataka wananchi kushirikiana na mkandarasi kwa shughuli ndogondogo kama za usafi katika eneo hilo.

Mhe Dk. Ndumbaro pia amemshukuru Mhe.Dk. Samia Suluhu Hassan,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha za miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Jimbo lake la Songea Mjini na kuahidi kusimamia miradi hiyo ili thamani ya fedha aliyoitoa Mhe Rais ionekane na ilete tija iliyokusudiwa.

“Mhe.Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan ametuletea Shilingi Bilioni Moja kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hii. Lakini mimi nilimuomba atuongezee fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi na kuifanya kuwa hospitali ya kisasa zaidi na Mhe Rais Dk. Samia akakubali na ametuongezea Shilingi Milioni 800.

Tunataka inapofika tarehe 1, Septemba huduma zianze kutolewa hasa hizo za awali hivyo lazima kasi iongezwe wananchi hawa waanze kupata huduma mapema zaidi,” amesisitiza Mhe Dk. Ndumbaro.

Amesema kuwa hospitali hiyo itakapokamilika kutakuwa na gari la kubebea wagonjwa, kutakuwa na huduma za upasuaji, maabara kubwa, wodi pamoja na mashine za kisasa za kutolea huduma na hivyo kuwaondolea adha wagonjwa waliokuwa wanalazimika kusafirishwa mikoa ya karibu kwa ajili ya matibabu.

About the author

mzalendoeditor