Kamishna wa Uhifadhi Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) William Mwakilema,akizungumza na Waandishi wa Habari leo Julai 24,2023 jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo na Mwelekeo wa utekelezaji wa Mwaka wa Fedha 2023/2024.
Waandishi wa habari wakifatilia hotuba ya Kamishna wa Uhifadhi Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) William Mwakilema (hayupo pichani), leo Julai 24,2023 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo na Mwelekeo wa utekelezaji wa Mwaka wa Fedha 2023/2024.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari -MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Gerson Msigwa, akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya Kamishna wa Uhifadhi Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) William Mwakilema,kuwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo na Mwelekeo wa utekelezaji wa Mwaka wa Fedha 2023/2024.
Na.Alex Sonna-DODOMA
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania(TANAPA),katika Mwaka wa fedha wa 2023/2024,limepanga kukusanya mapato ya shilingi bilioni 343.8 yatokanayo na vivutio mbalimbali vya utalii nchini.
Hayo yamesemwa leo Julai 24,2023 Jijini Dodoma na Kamishna wa Uhifadhi Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) William Mwakilema wakati akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo na Mwelekeo wa utekelezaji wa Mwaka wa Fedha 2023/2024.
“Katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2023 tulipanga kukusanya mapato kiasi cha Sh. bilioni 300 lakini kutokana na jitihada zizofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan za kuitangaza nchi ndani na nje na kupungu kwa makali ya UVIKO-19 tulikusanya bilioni 337 kiasi ambacho kilivunja rekodi ambayo hatujawahi kukusanya hapo awali”amesema Kamishna Mwakilema
Aidha amesema kuwa Shirika linaendelea kuimariha miundombinu mbalimbali katika hifadhi zote kwa msaada wa serikali pamoja na wadau wengine ikiwemo Benki ya Dunia.
“Hifadhi ambazo zinawatalii wengi hivi sasa ni zile za ukanda wa Kaskazini lakini lengo letu ni kuimarisha pia za kanda nyingine ambazo ni pamoja na ile ya Mikumi, Nyerere, Sadani, Mkomazi pamoja na Ruwaha ili kuongeza idadi ya watalii kufikia agizo la Ilani ya uchaguzi linalotaka ifikapo 2025/26 kuwa na watalii milioni tano na mapato yapatayo yatokanayo na utalii kiasai cha dola bilioni sita”amesema
Pia ametoa ombi kwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS),na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA),kurekebisha miundombinu ya barabara hasa ya kutoka Nagulo Chamwino hadi Ilangali ambayo ni njia ya fupi ya kuingia hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Vile Vile amesema mikakati mingine ni kulinda mito minne ambayo inatoka nje ya hifadhi za taifa ili kulinda ikolojia na kuwaondoa katika hatari wanyama ya kukosa maji kama itakauka kutokana na kuathiriwa na shughuli za kibinadamu.
“Kuna mito kama mnne hivi ambayo inatoka nje ya hifadhi za taifa mito hiyo ni pamoja na mto Mara ambao ni mto muhimu sana katika hifadhi ya Serengeti kiikolojia ambao kama hautalidwa na kukauka wanyama watakosa maji kwani hivi sasa itegemewa kutokana na kutililisha maji mwaka mzima”amesema Kamishna Mwakilema
Katika hatua nyingine amesema kuwa kwa mtu yeyote ambaye atapenda kumpa mnyama jina lake gharama zake ni Sh. milioni tano.
Amesema kuwa kumekuwepo na utaratibu wa wanyama mbalimbali walipo katika hifadhi za taifa kupatiwa majina ya watu kama vile Faru John na mengine mengi, hivyo kama kuna mtu ambaye anataka jina lake apatiwe mnyama gharama ni Sh. milioni tano.
“Kila mtu anaweza kumpatia mnyama jina lake ili alitumie kama utambulisho wake hifadhini, hivyo niwakaribishe watu wote ambao wangependa majina yao yao wapatiwe wanyama wetu katika hifadhi zetu ikiwa ni sehemu ya kuwalinda lakini gharama zake ni Sh. milioni tano,”amesema Kamishna Mwakilema
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari -MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Gerson Msigwa, amesema serikali ina mpango wa kujenga barabara ya kutoka Jiji la Dodoma,Bahi hadi Chamwino yenye urefu wa Kilomita 99 ambayo ndani yake ipo barabara hiyo ya Nagulo hadi Ilangali.
TANAPA ilianziswa mwaka 1959 ikiwa na majukumu mbalimbali ikiwemo kusimamia na kuendeleza maeneo yaliyoteuliwa kuwa hifadhi za Taifa kwa kuchukua hatua na kutumia njia za kuhifadhi urithi wa Taifa.