Morocco wameandika historia kwa kutwaa taji lao la kwanza la Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 23, AFCON U-23 kufuatia ushindi wa 2-1 dhidi ya waliokuwa wanashikilia Kombe hilo, Misri usiku wa kuamkia leo Uwanja wa Moulay Abdellah Jijini Rabat.
Katika mchezo huo uliohitaji dakika za nyongeza kuamua mshindi, Misri ilimaliza pungufu kufuatia beki wake, Mahmoud Saber kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 18 tu kwa kumchezea rafu Abdessamad Ezzalzouli.
Mahmoud Saber anayechezea klabu ya Ghazl El Mahalla ya nyumbani, Misri alitolewa kwa kadi nyekundu dakika nane tu tangu aifungie timu yake bao la kuongoza dakika ya 10 na ndipo Morocco ikatoka nyuma kwa mabao ya Yanis Begraoui dakika ya 37 na mtokea benchi Oussamna Targhalline dakika ya 105 kutwaa taji hilo.
Zote, Morocco na Misri zimejikatia tiketi ya kucheza Michezo ya Olimpiki mwakani Jijini Paris pamoja na Mali ambao wamepata nafasi hiyo baada ya kuifunga Guinea katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya 0-0 juzi.
Guinea nayo inaweza kufuzu kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris kama mwakilishi wa nne wa Afrika iwapo itashinda mechi ya mchujo dhidi ya mpinzani kutoka Bara la Asia ambaye bado hajajulikana.