Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Prof. Adolf Mkenda, akikagua Maendeleo ya mradi wa Kujenga Ujuzi kwa Maendeleo na Uingiliano wa Kikanda katika Afrika Mashariki (EASTRIP), unaotekelzwa katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Kampasi ya Mwanza.
Na,Mwandishi Wetu-MWANZA
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda, ameeleza kuridhishwa na maendeleo ya mradi wa Kujenga Ujuzi kwa Maendeleo na Uingiliano wa Kikanda katika Afrika Mashariki (EASTRIP), unaotekelzwa katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Kampasi ya Mwanza.
Mradi huo unaohusisha pamoja na mambo mengine, ujenzi wa jengo la taaluma, utawala na mabweni mawili, unafadhiliwa na Benki ya dunia kwa gharama ya Sh billioni 37.
“Nafurahi kusikia kwamba mkandarasi utamaliza kazi ndani ya mwaka huu ingawaje kwa muda huu uko nyuma ya kwa miezi miwili. Ongeza kasi ili uendelee kupata ‘tenda’ zingine hapa maana mradi huu unatekelezwa kwa awamu,” alisema.
Wakati huohuo aliishauri Kampasi kuzingatia suala la wanafunzi kubadilishana ujuzi na taasisi zingine za elimu nje ya Tanzania, ili kupata wataalam wa kutosha katika tasnia ya ngozi.
Alisema serikali imekua ikiingia mikataba ya makubalino (MoU) ya kubadilishana ujuzi na taasisi mbalimbali za elimu ya juu, ndani na nje ya Afrika, akaisistiza DIT kutumia fursa hiyo, ikizingatiwa Tanzania ina mifugo mingi ya kutoa malighafi kwa viwanda.
Kaimu Mkurugezi wa Kampuni ya Confix and engineering Limited, inayotekeleza mradi huo, Mhandisi Allan Magoma, alikiri mradi kuwa nyuma ya muda kwa miezi miwili, lakini kazi inafanyika usiku na mchana ili kuzipa pengo.
Alisema sababu za kuwa nyuma ni mvua zilizonyesha mfululizo siku kadhaa nyuma, pamoja na kubadilika kwa michoro kwa baadhi ya majengo.
“Ujenzi wa jengo hili la taaluma pamoja na mabweni yote utakamilika mwezi Oktoba, na wa jengo la utawala utakamilika mwezi Novemba,” alisema.
Akijibu swali la matunda tarajiwa ya mradi, Mkuu wa Kampasi, Albert Mmari, alisema usajili wa wanafunzi utaongezeka takribani mara 10, kutoka 200 wa sasa hadi 2,000.
Elimu kwa vitendo nayo itaboreshwa kwani mradi kwa ujumla wake (awamu ya kwanza na pili) utahusisha ujenzi wa kituo cha umahili wa uchakataji ngozi, kitakachokua na mashine za kisasa.