Featured Kitaifa

ICTC YATOA RAI KWA VIJANA WENYE BUNIFU ZA TEHAMA

Written by mzalendoeditor

 

MKURUGENZI wa Tume ya Tehama (ICTC), Dk. Nkundwe Mwasaga,akizungumza kuhusu mwamko wa vijana wenye bunifu na umuhimu wa Tume hiyo.

Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI wa Tume ya Tehama (ICTC), Dk. Nkundwe Mwasaga ametoa rai kwa vijana wenye bunifu za Tehama kufika katika Tume hiyo ili kupewa fursa mbalimbali ikiwamo tararibu za kuzisajili ili kulinda ubunifu wao.

Dk. Mwasaga ameyasema hayo Juni 26, 2023 alipokuwa akizungumzia kuhusu mwamko wa vijana wenye bunifu na umuhimu wa Tume hiyo.

“Dhamira ya serikali ni kuhakikisha vijana wanapata fursa za ndani na nje ya nchi, mikopo na hili tuliona tukuze kupitia vijana tangu tumeanza tumeona vijana wana uwezo mkubwa wa kubuni na wanajituma,”amesema.

Amesema Tume hiyo ina jukumu la kukuza bunifu zao. Katika kukuza bunifu zao ni vizuri wenye bunifu kuzisajili na Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA). Tume itaratibu mchakato huo.

“Nitoe rai kwa vijana wenye bunifu kuzisajili ili kuwa na uhakika kwamba hakuna atayeuchukua ubunifu wako bila ruhusa yako. Tume imetambua kuwa kikubwa zaidi kwamba kuna watu wanatoka nje ya nchi kwa nia ya kununua bunifu za vijana wa Tanzania lakini hawapendi kununua kitu ambacho hakijasajiliwa. Kwa mnunuzi ubunifu ambao haujasajiliwa unaweza kumjengea hali ya kuhisi umemuibia kutoka kwa mtu mwingine,”amesema.

Amesema watu wenye bunifu za Tehama wafike kwenye Tume hiyo ili kuwapa ushauri na kuwafungulia fursa za kunufaika na bunifu zao.

“Watu ambao wana mitaji na wapo tayari kutoa ili ubunifu ukue wapo na wapo wengine Tanzania wameshakuja kuniona mimi wapo wengi ila sasa bunifu kuwa katika hatua ambayo mtu anaweza kuweka fedha yake inatakiwa vitu vingine vifanyike.”

“Kuna kitu nimekiona kwa wabunifu wengi wana uwezo mkubwa sana katika kufanya vitu kwenye eneo la kiufundi kama kutengeneza mfumo na vitu vingine wanajua lakini eneo ambalo tunahitaji kuwasaidia zaidi ni eneo la biashara,”amesema.

Awali, ametaja sababu ya serikali kuanzishwa Tume hiyo ni kuwasaidia watanzania ikiwamo vijana wenye bunifu za Tehama

“Tume hii ina miaka nane tangu imeanzishwa na serikali. Tathmini ya sera ya kwanza ya TEHAMA ya Taifa ambayo ilitengenezwa mwaka 2003 iliyofanyika baada ya miaka 10. Tathmini ambayo iliangalua jinsi sera ilivyotekelezwa na changamito zingine za utekelezaji. Tathmini hiyo ilionyesha cha kwanza sera haikuwa na mwenyewe iliyopelekewa kila mmoja kuitekeleza kwa namna anavyojua,”amesema.

About the author

mzalendoeditor