Featured Kitaifa

WAZIRI GWAJIMA ATAKA WATOTO KUJILINDA DHIDI YA UKATILI WA MTANDAONI

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Maendeleo Ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum,Dkt Dorothy Gwajima akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika Mkoani Dodoma,leo Juni 16,2023.

Katibu mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wanawake na Makundi Maalum Dkt John Jingu akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika Mkoani Dodoma leo Juni 16,2023.

Mwakilishi wa shirika la umoja wa Mataifa (UNICEF) John George akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika Mkoani Dodoma leo Juni 16,2023.

Mwenyekiti wa baraza la watoto Nchini Raphael Charles akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika Mkoani Dodoma leo Juni 16,2023.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima akiimba na kucheza na watoto wimbo wa kuwahamasisha watoto kujikinga na ukatili wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika,Mkoani Dodoma leo Juni 16,2023.

Na.Alex Sonna-DODOMA

WAZIRI  wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema utafiti uliofanywa na Wizara kwa kushirikiana na UNICEF mwaka 2022 ulibainisha 67% ya watoto wenye umri kati ya miaka 12 hadi 17 wanatumia simu na kuwa  asilimia 4 kati yao wamefanyiwa ukatili.

Waziri Gwajima ameyasema hayo leo Juni 16,2023 jijini Dodoma  wakati  akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika.

”Tumeendelea kushuhudia ukiukwaji wa utu, heshima na haki za watoto katika mitandao ya kijamii kutokana na watoto kuhusika moja kwa moja na matumizi mabaya ya mitandao au wanajamii kutumia mitandao kudhalilisha watoto. ”amesema Dkt.Gwajima

Aidha amewaasa wazazi,walezi na jamii kwa ujumla,kuhakikisha wanasimamie haki za watoto  mkosaji wanaemalizana kindugu hataacha kufanya uhalifu huo, ataendelea na kwa wengine.

Amesema tabia ya ndugu na jamaa wa karibu kama vile baba, mjomba au kaka kuhusishwa na matukio ya ukatili dhidi ya watoto wao husababisha kukosekana kwa haki kutokana na kumalizana kindugu.

“Kupitia maadhimisho haya, natoa wito kwa wazazi au walezi na vyombo vinavyosimamia haki kuhakikisha kwamba watoto waliofanyiwa vitendo vya ukatili wanapata haki kulingana na sheria za nchi yetu.Vilevile nawaomba wazazi wanaume tujitokeze katika kusimamia maslahi ya watoto wetu”amesema Dkt.Gwajima

Aidha amesema kuwa Wizara inaendelea kuratibu utoaji wa huduma ya msaada wa kisaikolojia na kijamii kwa makundi yenye mahitaji maalum ikijumuisha  wahanga wa ukatili na jamii zinazoathiriwa na majanga mbalimbali ili kuwarejesha katika hali njema.

Waziri Gwajima amesema kuwa  katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Aprili 2023 kupitia Ofisi za Ustawi wa Jamii katika Halmashauri zote wamehudumiwa Wahanga wa vitendo vya ukatili 13,926 ambapo watoto ni 6,784 na Wahanga wa vitendo vya ukatili na usafirishaji haramu wa binadamu walikuwa 452 wanaume ni watano na wanawake ni 447.

“Takwimu hizo zinaonyesha bado kuna kazi kubwa ya kufanya kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ambapo, changamoto zilizopo zinachangiwa na kukosekana kwa ushirikiano kutoka baadhi ya wazazi au walezi, askari na wanajamii katika kuibua na kushughulikia vitendo vya ukatili kwa mujibu wa sheria. Bado wazazi au wanajamii hawatoi ushirikiano kwa maslahi yao binafsi.”amesema

Katika maadhimisho hayo, Waziri Dkt. Gwajima amezindua mwongozo wa kupinga ukatili wa watoto kwenye michezo, vitini vya mafunzo ya malezi ya watoto na Baraza la watoto Taifa.

Pia  ametoa vyeti kutambua mchango wa waliojitolea kuunga mkono Kampeni ya kupinga ukatili kwa akiwemo Mwenyekiti wa SMAUJATA Taifa Sospeter Bulugu na Wenyeviti wa SMAUJATA wa Mikoa.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa watoto (UNICEF) John George amesema jamii ina wajibu wa kuhakikisha mitandao ya kijamii inatumika kwa manufaa mazuri, huku akionya jamii kuacha kusambaza taarifa zao binafsi kwenye Mitandao.

Awali Mwenyekiti wa Baraza la Watoto Raphael Charles amesema Baraza hilo linatambua jitihada zinazofanywa na Serikali kuwalinda watoto ikiwemo kuanzishwa kwa Kamati mbalimbali za ulinzi na madawati ya Jinsia.

”Naiomba Serikali iendelee kushughulikia kilio cha Watoto dhidi ya ukatili wa mitandaoni kwa kuwachukulia hatua stahiki wale wote wanao wafanyia ukatili.”amesema Charles

Hata hivyo  amesema watoto pia wana wajibu wa kutoa taarifa wanapofanyiwa ukatili.

About the author

mzalendoeditor