Featured Kitaifa

RAIS SAMIA ANATARAJIA KUWA MGENI RASMI MAADHIMISHO SIKU YA USHIRIKA DUNIANI

Written by mzalendoeditor

 

 Mrajisi na Mtendaji Mkuu wa Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) , Dkt. Benson Ndiyege, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Juni 2,2023 jijini Dodoma kuhusu maadhimisho  ya Siku ya Ushirika Duniani yanayotarajia kufanyika kitaifa mkoani Tabora kuanzia Juni 26 hadi Julai 1, mwaka huu.

Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi kutoka Bw.Bahati Rukiko ,akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho  ya Siku ya Ushirika Duniani yanayotarajia kufanyika kitaifa mkoani Tabora kuanzia Juni 26 hadi Julai 1, mwaka huu leo Juni 2,2023 jijini Dodoma

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania, (TFC) Charles Jishuli,akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho  ya Siku ya Ushirika Duniani yanayotarajia kufanyika kitaifa mkoani Tabora kuanzia Juni 26 hadi Julai 1, mwaka huu leo Juni 2,2023 jijini Dodoma

Katibu Mtendaji wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania Bw.Alex Ndikilo,akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho  ya Siku ya Ushirika Duniani yanayotarajia kufanyika kitaifa mkoani Tabora kuanzia Juni 26 hadi Julai 1, mwaka huu leo Juni 2,2023 jijini Dodoma

Na.Alex Sonna-DODOMA

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya ushirika duniani yatakayofanyika  kitaifa mkoani Tabora.

Hayo yamesemwa leo Juni 2,2023 jijini Dodoma na Mrajisi na Mtendaji Mkuu wa Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) , Dkt. Benson Ndiyege, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho hayo yatakayofanyika kitaifa mkoani Tabora kuanzia Juni 26 hadi Julai 1, mwaka huu.

Dkt.Ndiyege amesema kuwa lengo la maadhimisho hayo  ni kuwakutanisha wadau wa ushirika wakiwemo viongozi wa ushirika, vyama vya ushirika, wadau wa ushirika na viongozi wa Serikali wanaosimamia sekta ya ushirika.

“Pia kutangaza kazi za wanaushirika, kuhabarisha umma juu ya falsafa na manufaa ya ushirika na kutoa fursa ya kujadili changamoto za kiuchumi na kijamii zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi. Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya Mwaka huu ni “Ushirika kwa Maendeleo Endelevu””amesema Dkt. Ndiyege

Aidha, amesema  maadhimisho hayo yataambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo makongamano, utoaji wa zawadi, Uchangiaji Damu, Upimaji wa Afya, Shindano la insha, Burudani na Michezo.

“Hii ni nafasi ya kuonesha bidhaa za wanaushirika, kazi za Wanaushirika na kuuenzi ushirika ili kufanikisha Ajenda ya Kimataifa – 2030 na Malengo Endelevu (Sustainable Development Goals – SDGs) kupitia Ushirika”amesema

Pia, amesema maadhimisho ya siku ya Ushirika Duniani hutoa fursa kwa wajasiriamali na wafanyabiashara kutoa huduma kwa washiriki na kupelekea kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja, uchumi wa Mkoa husika na Taifa kwa ujumla.

“Na hutoa fursa kwa wadau wa Maendeleo ya Ushirika kujifunza kuhusu fursa za uwekezaji na ufanyaji biashara kupitia bidhaa na mazao yanayozalishwa kwenye Vyama vya Ushirika’amesema Dkt. Ndiyege

Hata hivyo amesema kuwa maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani husaidia kuwaunganisha wanaushirika na wabia wa maendeleo toka ndani na nje ya nchi na kuviunganisha vyama vya ushirika ili kuimarisha mahusiano katika kusaidiana masuala ya kiuchumi na kijamii.

“Katika kufanikisha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani kwa mwaka huu, tunatoa wito kwa wanaushirika na wabia wa maendeleo toka ndani na nje ya nchi kushiriki kikamilifu kuonesha bidhaa na huduma zinazotolewa katika vyama vya ushirika na wadau wake”amesema

Aidha Dkt. Ndiyege amesema kuwa wamejipanga kuja na mfumo wa kidijitali utakao saidia kuweka uwazi kwenye vyama vya ushirika ili kukomesha viongozi ambao wamekuwa wakiendesha shughuli zao kiujanja ujanja.

“Mfumo huu ukifungwa utawezesha hata mimi nikiwa hapa ofisi naweza kuona ushirika wowote na kutoa maelekeo kabla ushirika ule haujakufa”amesema

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania, (TFC) Charles Jishuli, amesema kuwa ushirika umekuwa na tija kubwa nchini licha kuwepo kwa mitizamo hasi kwa baadhi ya watu.

“Ushirika ndiyo unasaidia kukua kwa sekta binafsi bila kuwepo kwa ushiriki ingekuwa kazi sana kwani kila mkulima angeuza zao lake nyumbani kwake hivyo ushirika ni muhimu sana katika taifa letu na hivi sasa wanachama wa ushirika wamefikia 8,000,000 nchini nzima”amesema Jishuli

About the author

mzalendoeditor