Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa Programu ya kuwainua wanawake kiuchumi “ANAWEZA” kwa niaba ya Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma Mei 31, 2023. Kushoto ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Riziki Pembe.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima,akizungumza wakati wa uzinduzi wa Programu ya kuwainua wanawake kiuchumi “ANAWEZA” kwa niaba ya Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango katika hafla iliyofanyika leo Mei 31,2023 jijini Dodoma.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Riziki Pembe akitoa salaam za Wizara hiyo wakati wa uzinduzi wa Programu ya kuwawezesha Wanawake kiuchumi ANAWEZA uliofanyika leo Mei 31,2023 jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) Afrika Mashariki, Jumoke Jagun Dokunmu akieleza jambo kuhusu programu ya ANAWEZA yenye lengo la kuwawezesha wanawake kiuchumi iliyozinduliwa leo Mei 31,2023 jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Fatuma Taufiq,akizungumza wakati wa uzinduzi wa Programu ya kuwainua wanawake kiuchumi “ANAWEZA” hafla iliyofanyika leo Mei 31,2023 jijini Dodoma.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri (ATE) Sussane Ndomba akizungumza wakati wa uzinduzi wa Programu ya uwezeshaji Wanawake ya ANAWEZA uliofanyika leo Mei 31,2023 jijini Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule akitoa salam za Mkoa huo kwa washiriki wa hafla ya uzinduzi wa programu ya kuwawezesha wanawake kiuchumi inayoitwa ANAWEZA, uliofanyika leo Mei 31,2023 jijini Dodoma.
Sehemu ya washiriki wakifatilia hotuba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima (hayupo pichani),wakati wa uzinduzi wa Programu ya kuwainua wanawake kiuchumi “ANAWEZA” kwa niaba ya Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango katika hafla iliyofanyika leo Mei 31,2023 jijini Dodoma.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuzindua Programu ya kuwainua wanawake kiuchumi “ANAWEZA” kwa niaba ya Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango katika hafla iliyofanyika leo Mei 31,2023 jijini Dodoma.
Na Dotto Kwilasa, Dodoma.
Serikali kwa kushirikiana na Taasisi ya Benki ya Dunia (IFC) imezindua programu mpya ya Jinsia inayojulikana kama “Anaweza” kwa lengo la kuwawezesha wanawake kiuchumi itakayo tekelezwa kwa miaka mitano na kugharimu Dola za kimarekani milioni 10.
Akizungumza leo Mei 31,2023 Jijini Dodoma kwenye uzinduzi huo,Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na makundi maalumu Dkt.Doroth Gwajima IFC ikiwa ni Taasisi tanzu ya Benki ya Dunia ina lengo la kuwezesha wananchi kiuchumi na kuachana na utegemezi.
Katika kuunga mkono juhudi hizo Waziri Gwajima amesema hadi kufikia Aprili mwaka huu serikali ilikuwa imetoa sh.bilioni 30.9 kwa vikundi 5,120 vya wanawakea katika Halmashauri 184 nchini.
Fedha hizo zimetolewa Kwa lengo la kuboresha kipato na kuondoa umaskini kwa wanawake na wanaume nchini.
Amesema kupitia sheria ya fedha za mamlaka za serikali za mitaa ya mwaka 2018 inayozitaka Halmashauri zote nchini kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo isiyo na riba kwa Makundi maalum ikiwemo wanawake asilimia nne, vijana asilimia nne na watu wenye ulemavu asilimia mbili.
Dk.Gwajima ameeleza kuwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF) unaosimamiwa na wizara anayoisimamia imetoa mikopo yenye thamani ya sh.milioni 664.5 kwa wanawake wajasiriamali 104 katika kipindi cha Julai 2022 hadi Aprili,mwaka huu.
“Tanzania ni miongoni mwa Mataifa yanayotekeleza malengo ya jukwaa la kimataifa ya kukuza usawa wa kijinsia ambapo Rais Dk. Samia ni kinara wa utekelezaji wa Jukwaa hilo hususan kuhusu haki na usawa wa Kiuchumi,tumetengeneza programu inayotekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali na Sekta binafsi ili ifikiapo mwaka 2026 hali ya Wanawake iwe imebadilika kwa kiasi kikubwa,”amesema
Pamoja na jitihada hizo amesema Programu hiyo iliyozinduliwa inajumuisha kutengeneza mazingira bora ya malezi ya awali na uangalizi wa watoto katika ngazi ya jamii ikiwemo masokoni lakini pia katika maofisi ili kuhakikisha huduma za msingi kama vile maji na umeme zinafika kwa ukamilifu vijijini ili kutatua changamoto zinazowakumba wanawake,”alieleza
Amefafanua kuwa Programu ya ANAWEZA itachangia kufanikisha utekelezaji programu wa kizazi chenye usawa hapa nchini na kuwezesha wanawake kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi
“Ni matarajio yangu kuwa mpango utashirikisha sekta binafsi hapa nchini ili kukuza upatikanaji wa fursa za wanawake katika nafasi za uongozi na ajira bora ili kuchochea ukuaji wa uchumi nchini;
Utafiti unaonyesha kuwa kuziba pengo la kijinsia kati ya ajira za wanaume na wanawake kunaweza kuongeza Pato la Taifa la muda mrefu kwa kila mtu kwa asilimia 4.8.
Kwa upande wake Mkurugenzi Kanda wa IFC Jumoke Jagun-Dokunmu, alisema program ya ANAWEZA itatekelezwa kwa miaka mitano na inalenga kushughulikia changamoto zilizopo ili kuwezesha ushiriki wa wanawake katika sekta binafsi, nafasi za uongozi na ujasiriamali wenye ufanisi endelevu.
Amesema programu hiyo itakagharimu fedha za Kimarekani milioni 7.5, inaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
“Wanawake wanaweza kuwa injini ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania, hivyo kuwawezesha wanawake kunachukua jukumu kubwa la kukuza uchumi na kuwezesha upatikanaji wa maisha bora kwa watu binafsi na familia zao” amesema.
Katika kusisitiza hilo amesema hakuna nchi inayoweza kupata maendeleo bila mwanamke na hivyo kupitia Uwekezaji huo Tanzania inaenda kuwa kinara na mfano wa kuigwa na mataifa mengine kuhusu uwezeshaji wanawake.
“Tunajipanga kusaidia wanawake wengi zaidi kupata Mafanikio kiuchumi ,tutafanya pia na sekta binafsi kuwekeza kwenye kilimo kuongeza ufanisi wa Wanawake kwenye masuala ya kiuchumi na kuweka usawa kwenye masuala ya jinsia,”anasisitiza
Amefafanua kwa tathmini ya Benki ya Dunia ya mwaka 2022 kuhusu hali ya jinsia Tanzania inaonyesha kuwa imepiga hatua katika kuongeza usawa wa kijinsia kwa kufanya jitihada za kukabiliana na ukosefu wa usawa wa kijinsia katika Nyanja zote za maisha ya wanawake.
Naye Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Riziki Pembe amesema kuwa Serikali ya Muungano inathamini kazi zinazofanywa na wanawake Katika kuchochea maendeleo ya uchumi hivyo imekuwa akiwateu kushika nafasi mbalimbali za uongozi.
“Tunatambua juhudi za wanawake katika uongozi na sisi tupo nyuma yenu kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma,lazima tushirikiane kufika mbali zaidi,”anasisitiza