Featured Kitaifa

SERIKALI ZOTE MBILI ZA TANZANIA NA TAASISI ZAKE KUIMARISHA MASHIRIKIANO SEKTA YA KILIMO,MALIASILI NA MIFUGO

Written by mzalendoeditor

 

Mhifadhi wa msitu wa Jane Goodall uliopo Pugu jijini Dar es salam, Rashid Mustafa (kushoto) akitoa maelezo kwa viongozi wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar walipotembelea msitu huo wakati wa ziara ya kujifunza inayoongozwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Seif Shaaban Mwinyi (wa tatu kulia).

Mhifadhi wa msitu wa Jane Goodall uliopo Pugu jijini Dar es salam, Rashid Mustafa (kushoto) akiwaongoza viongozi wa wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar walipotembelea msitu huo wakati wa ziara ya kujifunza inayoongozwa na katibu mkuu wa wizara hiyo, Seif Shaaban Mwinyi.

NA SALAMA MOHAMED, WKUMM

KATIBU Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Seif Shaaban Mwinyi, amesema serikali zote mbili za Tanzania na taasisi zake zitaendelea kuimarisha mashirikiano ili ziweze kuleta maendeleo nchini.

Akizungumza katika hifadhi ya Msitu Pugu kanda ya Mashariki wilaya ya Ilala, Dar es salam wakati wa ziara ya kutembelea msitu wa Jane Goodall iliyojumuisha viongozi na watendaji wa Wizara hiyo.

Amesema dhamira ya ziara hiyo ni kuongeza mashirikiano na kujifunza mazingira yaliopo katika msitu huo ambapo taasisi hiyo imeweza kupiga hatua ya maendeleo katika kuwainua vijana kujifunza mbinu mbali mbali za hifadhi ya misitu.

Seif ameeleza kuwa uwepo wa msitu huo umeongeza tija kwa kupata mashirikiano mazuri na wanajamii waliozunguka maeneo hayo kwa kufanya miradi yenye kuwapatia tija kutokana na hifadhi hiyo.

Nae Msimamizi wa Jane msitu Goodall, Rashid Mustafa, amesema msitu huo una vivutio vingi ikiwemo aina 36 za wanyama, ndege 235 na aina 414 za miti na mimea.

Mbali na uwepo wa ndege na wanyama hao pia eneo hilo linatumika kwa tafiti mbali mbali zinazoshirikisha vyuo vikuu vya Tanzania wakiwemo wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine na chuo kikuu cha Dar es salaam na vyuo vikuu vya nje ya nchi.

Kwa mujibu wa wahifadhi wa hifadhi ya msitu wa Pugu, walieleza hifadhi hiyo imeanzishwa na Jane Goodall mnamo mwaka 2017 ikiwa na ukubwa wa hekta 6 na kupewa jina la Nature Center kwa ajili ya mafunzo kwa klabu na jumuiya za uhifadhi za ndani na nje ya nchi kwa ajili ya uhifadhi endelevu.

Ziara hiyo ni matokeo ya ushirikiano wa muda mrefu kati ya Jane Goodall na Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar katika kusimamia na kuendeleza hifadhi za misitu ya Jambiani na Muyuni ambapo matarajio ya ujumbe huo kujifunza zaidi katika mwendelezo wa ziara hiyo itakayowafikisha mkoani Kigoma.

About the author

mzalendoeditor