MKUU wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU), Mkoa wa Dodoma,Bw.John Joseph wakati ,akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Mei 26,2023 jijini Dodoma kuhusu taarifa ya miezi mitatu za kazi za Taasisi hiyo.
Na.Alex Sonna-DODOMA
KATIKA kipindi cha Miezi mitatu kuanzia Januari 1 hadi Machi 31 mwaka huu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU), Mkoa wa Dodoma imefuatilia miradi 36 yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 16 katika sekta za elimu, afya, Ardhi, Kilimo, ujenzi, barabara na fedha .
Hayo yamesemwa leo ,Mei 26 ,2023 jijini Dodoma na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma,Bw.John Joseph wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa ya miezi mitatu za kazi za Taasisi hiyo.
Amesema jumla ya miradi 22 ya elimu imefanyiwa ufuatiliaji, Kilimo miradi 5,fedha 3 na afya miradi 4 hali iliyosaidia kufikia fedha kiasi cha shilingi 1,050,000 katika Wilaya ya Chamwino.
“Miradi 21 imetolewa ushauri na elimu pia ufuatiliaji unaendelea, miradi 7 imekamilika ,miwili imetolewa maelekezo, chambuzi za mifumo ya warsha miradi miwili,miradi miwili inaendelea na ufuatiliaji nyaraka katika Wilaya ya Chamwino,”amesema Bw.Joseph
Aidha Bw.Joseph amesema kuwa wamepokea malalamiko 138 kati ya malalamiko hayo ,malalamiko 81 yalikuwa ya Rushwa na walalamikaji walielimishwa na kupewa ushauri wengine saba taarifa zake zimehamishiwa idara nyingine kwa hatua zaidi.
Amesema kuwa kati ya malalamiko hayo,malalamiko 57 yalihusu rushwa ambayo yalipelekwa kufunguliwa majalada ya uchunguzi.
”Kati ya majalada hayo 57 uchunguzi wa majalada 17 umekamilika,mashauri mawili yamefunguliwa mahakamani na majalada 15 hatua mbalimbali za kisheria zinatarajiwa kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa huku majalada 40 uchunguzi wake bado unaendelea na uko katika hatua mbalimbali za kiuchunguzi.”amesema
Ametaja idara zinazolalamikiwa kutokana na taarifa 57 ni huku elimu ikiongoza kwa malalamiko 11,TAMISEMI malalamiko tisa,sekta binafsi tisa ,Ardhi saba ,Afya saba ,polisi tano,kilimo tatu,manunuzi mawawili ,mahakama moja,maji moja,mazingira moja na fedha moja.
“Mashauri mapya manne yametolewa maamuzi ambapo hadi sasa mashauri mawili tumeshinda na mashauri tumeshindwa na jumla ya mashauri 31 yanaendelea kusiilizwa mkoani hapa na yako katika hatua mbalimbali,”amesema.
Hata hivyo amesema kuwa wameweza kudhibiti jumla ya Shilingi milioni 41.2 ambazo zilikuwa kayika hatari ya kufanyiwa ubadhirifu katika fedha za mpango wa maenedeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uviko 19.
Pamoja na hayo ametaja vipaumbele kwa kipindi kinachofuata cha mwezi Aprili hadi Juni mwaka huu ambapo amesema wataongeza kasi ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuziba mianya ya rushwa na ufujaji.
Pia Kuongeza kasi ya uelelimishaji umma kwa kutumia njia mbalimbali,kuongeza kasi katika kufanya chambuzi za mfumo hasa katika maeneo yanayolalamikiwa zaidi na kuendelea kuelimisha jamii na hususani kundi la vijana kupitia ushirikiano uliopo kati ya TAKUKURU na SKAUT-TAKUSKA na jamii nzima ya wana Dodoma.
Aidha amewataka Wakurugenzi wa halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma pamoja na Madiwani wote kufuatilia kwa karibu miradi ya maendeleo iliyo katika maeneo yao kwani baadhi ya wakandarasi pamoja na kupewa malipo ya awali lakini hawawendi kufanya kazi walizoomba.