Featured Kitaifa

BANDARI YA DAR ES SALAAM IBORESHWE _MBUNGE MTATURU

Written by mzalendoeditor

MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amesema Bandari ya Dar es Salaam kijiografia imekaa vizuri na ikitumiwa vizuri italeta mapato mengi kuliko eneo lolote.

Mtaturu amesema hayo Mei 22,2023,Bungeni Jijini Dodoma wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

“Pamoja na uzuri huu bado bandari hii haitoi mchango wa kutosha,tumeboresha sana gati namba 8 mpaka 11,tumejitahidi kuongeza masuala ya usalama katika bandari ni sawa,lakini tumeongeza Crane mbili ambazo zinafanya kazi,na tukiangalia Bandari nyingine kama kule Mundra India,Dubai na nchi nyingine Bandari zake zinafanya kazi vizuri,

“Pia tumeongeza mapato Bilioni 700 hadi Trilioni moja tu ambayo kimsingi ukiangalia hizi fedha bado ni ndogo kwa bandari yetu ilivyokaa,nchi nane zinategemea Bandari ya Dar es Salaam,hivyo tukiboresha vizuri itakuwa nijibu ya fedha ambazo hatuzipati katika eneo hilo,

Ameiomba serikali kuangalia changamoto ziliopo ikiwa ni pamoja na kutokuwa na mifumo ya kusomana ambayo inaweza kumvutia mteja kuvutika kuja kufanya biashara.

“Niombe tuhakikishe tunaleta mwekezaji atakayeshirikiana na serikali, sio dhambi,uwekezaji wa pamoja ( PPP), imetajwa kwenye sheria zetu,tusiwe waoga watanzania tunapotaka kubadilisha maisha ya wananchi wetu,tuhakikishe kwamba tunaweza kubadilisha na kuongeza uchumi wa nchi yetu kusaidia Taifa hili ili tuweze kujenga madarasa na miundombinu mbalimbali kwa ajili ya maisha ya watanzania,”amesema.

PONGEZI KWA RAIS SAMIA.

Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya ikiwemo kuridhia fedha nyingi kwenda kwenye wizara hiyo ambayo inaendesha na kusukuma uchumi wa Tanzania.

“Wizara hii ndio imebeba daraja la uchumi wa nchi yetu na imebeba mabadiliko ya uchumi ambao tunautarajia,nimpongeze Rais wetu kwa kazi nzuri anayoifanya katika kujenga barabara,miundombinu,reli, tunanunua meli,tunanunua ndege na kadhalika ,kazi hii inafanyika vizuri na ataandikwa kwenye kitabu cha dhahabu,”amebainisha.

Amempongeza pia Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa na watendaji wake wote kwa kazi kubwa wanayoifanya,“ bahati nzuri sisi wengine wajumbe wa kamati ya miundombinu tunaona kazi nzuri inayofanywa,TANROADS iliyopewa dhamana ya kuunganisha barabara kuu za mikoa na wilaya kwa wilaya inafanya kazi nzuri sana,”

Amesema wizara hiyo wanawasimamia wakandarasi katika maeneo mbalimbali kujenga barabara, kujenga madaraja makubwa na madogo na kusimamia miundombinu mbalimbali nchini jambo ambalo ni lakupongezwa.

“Kwa mujibu wa utaratibu tuliojiwekea ni kuunganisha barabara za mikoa na mikoa,nipongeze sana utaratibu mpya ambao umeanzishwa wa kujenga barabara kwa mfumo mpya wa EPC + F,mfumo huu utaenda kuwa jibu la barabara ambazo hazikuwa zimekamilika kwa muda mrefu,”amesisitiza.

About the author

mzalendoeditor