Washiriki wa Mkutano wa Kamati Tendaji ya “Project ECHO” Tanzania, iliyo chini ya Wizara ya Afya, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kikao hicho kumalizika, Dodoma hivi karibuni.
Mwenyekiti Bi. Mary Mtui (wa kwanza kulia), akiendesha kikao cha Kamati Tendaji ya Project ECHO Tanzania, Dodoma. Katikati ni Mratibu wa Project ECHO Tanzania Bw. Jacob Lusekelo, ambaye pia ni katibu wa Kamati hiyo. Kulia ni Bw. Victor Muchunguzi, mshauri wa Mafunzo na Machapisho kutoka Mradi wa ECHO, Chuo Kikuu Mzumbe.
Bi. Osigele Oswald kutoka Wizaya ya Afya, akichangia jambo wakati wa mkutano wa Kamati Tendaji ya Project ECHO Tanzania.
Bw. Victor Muchunguzi, mshauri wa Mafunzo na Machapisho kutoka Mradi wa ECHO, Chuo Kikuu Mzumbe akichangia jambo wakati wa mkutano.
Baadhi ya wajumbe wa mkutano wa Kamati Tendaji ya Project ECHO Tanzania, wakifuatilia kwa makini wasilisho wakati wa kikao kilichofanyika Hoteli ya Morena, Dodoma hivi karibuni.
Na.Mwandishi Wetu-DODOMA
Kamati Tendaji ya “Project ECHO” Tanzania, iliyo chini ya Wizara ya Afya, imekutana Dodoma katika kikao chake cha 13, kilichofanyika katika Hoteli ya Morena na kuwakutanisha wadau mbalimbali katika Sekta ya Afya wakiwemo wataalamu kutoka TAMISEMI, Wizara ya Afya, Wataalamu wa Maabara, wadau wa maendeleo katika Sekta ya Afya na wataalam kutoka mabaraza ya wataam (Professional councils), Chuo kikuu Mzumbe na wafadhili wa Mradi (CDC).
Kikao hicho kilifunguliwa na Mwenyekiti Bi. Mary Mtui, Msajili wa Baraza la Wataalamu wa Maabara akimwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali. Akizungumza katika mahojiano maalumu baada ya kikao hicho kumalizika, Bi Mary, amesema Kamati imefarijika kuona ongezeko la wataalamu wa afya wanaoshiriki katika mafunzo kwa njia ya mtandao, yanayotolewa katika vituo 9 (Hubs) zilizofungungiliwa nchini nzima.
“ Inatia moyo kuona idadi ya washiriki wa mafunzo inaongezeka kila siku, na hii inatokana na jitihada kubwa zilizofanywa na wataalamu wa Chuo Kikuu Mzumbe kupitia mradi wa Kuboresha mifumo ya Afya nchini unaofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia CDC. Kikubwa Mzumbe waongeze kasi ya kutoa CPD Points kwa washiriki” Alisema
Amesema ongezeko hilo linatokana na kutolewa kwa “CPD point” zinazowaongezea washiriki nafasi ya kuhuisha leseni zao, na baadhi kupanda madaraja; na hivyo kuwataka Chuo Kikuu Mzumbe kuongeza kasi ya kutoa CPD points kwa wakati, ili kuongeza idadi wa washiriki wa mafunzo ambayo yamekuwa yana manufaa makubwa katika kuboresha utoaji huduma za Afya nchini.
Miongoni mwa mafunzo yanayotolewa kwa sasa ni pamoja na kliniki za “Adult HIV, Pediatric HIV, MDR TB, HVL, HIV LAB, Supply Chain na AMS/IPC ECHO”. Hadi kikao cha 13 cha mwaka cha Kamati ya Utendaji, inakadiriwa zaidi ya CPD pointi 1600 zimetolewa kwa watumishi wa afya ambao wamekuwa wakipata mafunzo kwa njia hiyo ya mtandao, huku zaidi ya watumishi na watoa huduma za afya 650 wakishiriki mafunzo nchini nzima kila wiki. Kwasasa Mzumbe kwa kushirikiana na MCT, wanaendelea kuchakata maombi mapya ya CPD’s zaidi ya 2600 kwa washiriki waliokidhi vigezo vya ushiriki kwenye mafunzo.
Pamoja na mambo mengine kikao hicho, kimekusudia kujadili na kuweka mikakati ya namna ya kuongeza ushiriki wa wataalamu wa Afya katika mafunzo kwa njia ya mtandao “ECHO Platforms” pamoja kutolewa CPD point kwa wakati. Kwasasa mafunzo hayo yanaendeshwa kila wiki kupitia vituo 9 (hubs), na washiriki kufuatilia mafunzo hayo kupitia clinic (Spokes) zaidi ya 399 zilizofungiwa vifaa vya mafunzo nchi nzima.
Wakichangia mkutano huo, wadau wamepongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya na Wadau wa maendeleo CDC, kwa kuwekeza katika mfumo wa mafunzo kwa njia ya mtandao; na hivyo kuwajengea uwezo wataalamu wa Afya wakiwa mahali pa kazi.
Akieleza mikakati zaidi ya Wizara; Mratibu wa Project ECHO Tanzania Bw. Jacob Lusekelo amesema, Wizara inakusudia kuendelea kushirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali wa maendeleo nchini ili kupanua wigo wa mafunzo na usimamizi nchini katika kutoa mafunzo, miongozo na usimamizi wa wataalamu wa huduma za afya (immersion training).
Mkutano huo wa siku moja umefadhiliwa na Serikali ya Watu wa Marekeni, kupitia Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani katika kupambana na Ukimwi(PEPFAR) kipitia CDC na kuhudhuriwa na viongozi kutoka Wizara ya Afya, TAMISEMI, wawakilishi kutoka Mabaraza ya Kitaaluma Tanzania, Chuo Kikuu Mzumbe, MDH, THPS, MNH na NBTS. Mradi huu kwa sasa unatekelezwa na Chuo Kikuu Mzumbe.