Featured Kitaifa

KAYA 10,000 ZANUFAIKA NA TASAF WILAYANI SAME

Written by mzalendoeditor

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Annastazia Tutuba amesema kumekuwa na mafanikio makubwa katika utekelezaji wa miradi kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF kuanzia mwaka 2015 wakati Mpango unaanza utekelezaji wilayani humo

Amesema miongoni mwa mafanikio hayo ni wananchi kuwa na kipato na hivyo kuweza kujikimu, kuanzisha miradi mbalimbali na kuwajengea uwezo wananchi wa namna ya kuibua miradi ya kujikwamua kiuchumi.

Wilaya ya Same ina kata 34 na vijiji 103 zenye kaya 10,000 zinazonufaika na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini. Mkurugenzi Tutuba alieleza pia kuwa katika utekelezaji wa TASAF makundi ya watu wote wenye uhitaji yamefikiwa na kupitia maboresho yaliyofanyika kumeongezwa ruzuku kwa ajili ya watu wenye ulemavu.

“TASAF imefanya jambo kubwa kuwagusa watu wenye ulemavu ili waweze kupata mahitaji ya msingi na fedha za kuanzisha miradi ya kujiongezea kipato,” alisema Tutuba.
Kupitia utekekezaji wa miradi mbali mbali, Mkurugenzi Tutuba amesema kwamba miradi na shughuli nyingine wanazofanya walengwa zimewajengea uwezo wa kuibua miradi, kuitekeleza na kupata ujuzi ambao wanautumia katika maisha yao ya kila siku

“Wamejiandaa vilivyo hata watakapoondolewa kwenye Mpango wamepata ujuzi wa kuibua miradi ya kujiendeleza kwa kutumia nguvu kazi iliyopo katika jamii yao,” alisema Tutuba.

Wilaya ya Same imeshapokea shilingi bilioni 4 ambazo zimelipwa kama ruzuku kwa walengwa 10,000. Walegwa hao wanaunganishwa katika vikundi vya kuweka akiba na kuwekeza ili kuwa na kipato endelevu.

About the author

mzalendoeditor