Featured Kitaifa

WATAALAM WA ARDHI NA MAAFISA WAANDAMIZI JIJI LA DODOMA KUWEKA KAMBI NDACHI KUTATUA MIGOGORO YA ARDHI

Written by mzalendoeditor

 

Na. Dennis Gondwe, DODOMA

WATAALAM wa Ardhi na maafisa waandamizi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wataweka kambi katika Mtaa wa Ndachi uliopo Kata ya Mnadani kusikiliza na kutatua migogoro ya Ardhi kwa siku 21 ili wananchi waweze kuendeleza maeneo yao.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alipofanya mkutano wa hadhara kusikiliza na kutatua migogoro ya Ardhi kwa wananchi wa Mtaa wa Ndachi uliopo Kata ya Mnadani jijini hapa.

Mafuru alisema kuwa Jiji la Dodoma limekuwa likipokea malalamiko mengi sana ya Ardhi kutoka kwa wananchi wa Ndachi ambayo yamekuwa yakipelekwa kwa namna tofautitofauti. “Ndugu zangu wa Ndachi tumekuwa tukipokea malalamiko mengi sana, kuna wanaokuja moja kwa moja ofisini, wanaotuma barua, wanaokwenda mkoani na Wizara ya Ardhi Mtumba.

Tutaweka kambi siku 21, naamini tukikaa Ndachi kwa muda wa siku 21 hakuna kitu tutakiacha. Ndachi nitaweka wataalam wanne ambao sio kutoka Ardhi, wawili watakuwa wa sheria wengine watakuwa kutoka Maendeleo ya Jamii na Mazingira. Naleta watu ambao sio maafisa wa ardhi ili wawe ‘neutral’ wasifanye kazi kwa kushawishiwa na wataalam wa Ardhi, tutafanya kazi kwa siku tano halafu tutakutana kwaajili ya mkutano wa tathmini” alisema Mafuru.

Aidha, alielezea namna zoezi hilo la kutatua migogoro ya Ardhi Mtaa wa Ndachi linavyoenda kutekelezwa. “Tunamabalozi 86 na wanaaminika sana. Mabalozi ndio wanajua watu wao wote, wanajua nani kahudumiwa na nani hajahudumiwa, tunaenda kushirikiana nao watusaidie kumalizia hatua ya mwisho ya ugawaji. Tutaanza na Mtaa wa Ndachi, tutagawa timu mbili, timu moja eneo la Matuli na nyingine Ndachi. Tutakaa kwa siku tano, wenye changamoto kuanzia leo mkajiorodheshe kwa mabalozi wenu ndani ya siku hizo njoo na lalamiko lako lolote iwe mipaka, ‘invoice’, mapunjo ya asilimia za ugawanaji wa viwanja njoo na kitu chochote usichoridhika nacho. Tutaenda kuongeza kasi ya utoaji wa hati ndani ya hizo siku tano tukimaliza tutahamia Mtaa wa Mbwanga na Karume.

Akitoa malalamiko yake kwenye mkutano huo mkazi wa Ndachi, Abilai Sharifu alisema “Mkurugenzi ondoa wote unda kamati mpya kama kamati itaendelea kubaki na kuwa na watu walewale hatuwezi kupata haki sababu kamati hiyo ndio wapigaji wakuu. Kwanza kwenye Kamati ya Ardhi kuna wengine wameingia wanasiku 20 tu, sisi ndio wanandachi hatuwezi kutatuliwa matatizo yetu na mtu asiye mkazi wa Ndachi matatizo ya wananchi wa ndachi yatatatuliwa na mwanandachi. Ni ombi langu Mkurugenzi uvunje kamati yote sababu hawajachaguliwa na wananchi wa Ndachi.

Wakati huohuo Mkazi wa Matuli, Mohamed Mamba alisema kuwa migogoro ya ardhi kwenye Mtaa wa Ndachi haiwezi kuisha kama wananchi hawatashirikishwa katika kuunda kamati itakayosimamia matatizo yao.   “Ukitaka hii hali iishe kila sehemu ya mji wa Dodoma weka kamati itakayochaguliwa na wananchi wenyewe wanaowaamini sio wanachaguliwa na viongozi. Kamati ndizo zitashughulikia migogoro ya ardhi, unda kamati kila mtaa watakayoikubali wananchi kwa idadi itakayotakiwa uitambue na mtaa uitambue kamati hiyo ndio ipewe jukumu lakusimamia zoezi la ugawaji wa viwanja” alisema Mamba.

Akielezea historia ya mradi wa upimaji Ardhi Ndachi Afisa Upimaji Ardhi Jiji la Dodoma, Luis Kiwale alisema kuwa mradi wa upimaji wa ardhi Ndachi ulianza rasmi 2018 ukihusisha zoezi la uhakiki, upangaji, upimaji na sasa mradi upo kwenye hatua ya mwisho ya ugawaji. Zoezi la ugawaji wa viwanja kwenye Mtaa wa Ndachi linahusisha watu wa aina mbili ambao wote ni wanufaika wa mradi, kuna wamiliki wa mashamba na wananchi wazawa.

About the author

mzalendoeditor