Kamishna Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Dionisia Mjema akifungua kikaokazi cha kuainisha mahitaji ya mfumo wa kielektroniki wa usajili na usimamizi wa Mifuko na Programu za uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kilichofanyika jijini Dodoma.
Msaidizi wa Mipango na Mawasiliano, kutoka Mfuko wa Uhifadhi wa Milima ya Tao la Mashariki, Bw. Alan Kimbita, akiwasilisha mada katika kikao kazi cha kuainisha mahitaji ya mfumo wa kielektroniki wa usajili na usimamizi wa Mifuko na Programu za uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kilichofanyika jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki wa kikaokazi cha kuainisha mahitaji ya mfumo wa kielektroniki wa usajili na usimamizi wa Mifuko na Programu za uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kilichofanyika jijini Dodoma.
Afisa Mwandamizi, Usimamizi wa Fedha za Uwakala kutoka Benki ya Maendeleo TIB, Bw. Kenneth Lusesa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mifuko na Programu za Serikali ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa kipindi kinachoishia Machi 2023 katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma.
Kamishna Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha, Bi. Dionisia Mjema akifafanua jambo katika kikaokazi cha kuainisha mahitaji ya mfumo wa kielektroniki wa usajili na usimamizi wa Mifuko na Programu za uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kilichofanyika jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha na Mipango – Dodoma)
Na Farida Ramadhani, WFM – Dodoma
Serikali inaada mfumo wa kielektroniki wa Huduma Ndogo za Fedha ili kuboresha ufanisi wa usimamizi wa Mifuko na Programu za Uwezeshaji wananchi Kiuchumi.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Kamishna Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Dionisia Mjema, wakati akifungua kikaokazi cha kuainisha mahitaji yanayopaswa kuwekwa kwenye mfumo huo.
Alisema mfumo huo utawezesha upatikanaji wa taarifa sahihi za usajili, usimamizi na za kiutendaji zinazohusiana na usimamizi, utoaji mikopo, ruzuku na dhamana ya mikopo iliyotolewa kwenye Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.
“Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na wadau wengine ilijadili namna bora ya kuandaa Mfumo wa Huduma Ndogo za Fedha ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2017, Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 pamoja na Kanuni zake”, alibainisha Bi. Mjema.
Alisema katika hatua ya kwanza ya uandaaji wa Mfumo huo, Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Timu ya Wataalamu ilifanya mapitio ya mifumo yote iliyopo katika Sekta ya Huduma Ndogo za Fedha ikiwemo Mfumo wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) unaotumika katika usajili na usimamizi wa taasisi zinazopokea amana na zisizopokea amana unaoitwa Banking Supervision Information System (BSIS) na Mfumo wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania wa usajili na usimamizi wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) unaoitwa Cooperative Supervision Management Information System (CSMIS).
“Mfumo wa Benki Kuu ya Tanzania wa usajili wa Vikundi vya Kijamii vya Huduma Ndogo za Fedha unaoitwa Community Microfinance Groups Online Registration System, Mfumo wa utoaji mikopo na usimamizi wa fedha asilimia kumi (10%) ya mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) wa Ten Percent Loans Management Information System (TPLMIS) na Kanzidata ya uwezeshaji wananchi kiuchumi (Economic Empowerment Database) ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi”, aliongeza Bi. Mjema.
Alisema wakati wa kupitia mifumo hii ilibainika uwepo wa mifumo mingi ya utoaji taarifa ambayo haisomani hivyo ikapendekeza kutengeneza mfumo wa Sekta ya Huduma Ndogo za Fedha ambao utaiwezesha Serikali kuwa na taarifa sahihi za uwezeshaji wananchi na kuweza kuandaa mipango mbalimbali ya maendeleo.
Kwa upande wao washiriki wa kikaokazi hicho wameishukuru Serikali kwa kuamua kuandaa mfumo huo ambao kwa kiasi kikubwa utasaidia kutatua changamoto mbalimbali za uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Walibainisha changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa mifumo ya kidigitali ya upatikanaji wa taarifa na ongezeko la mikopo chechefu, ambayo inapunguza ufanisi katika usimamizi na utekelezaji wa shughuli za mifuko hiyo, ukosefu wa taarifa kwa wakati na baadhi kutofikiwa malengo ya uanzishwaji wake.