Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Mkewe Mary wakiweka shada la maua kwenye kaburi la marehemu Bernard Membe wakati alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye ibada ya mazishi ya Marehemu Membe yaliyofanyika kijijini kwake, Rondo, Chiponda Mkoani Lindi. Mei 16, 2023 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Mkewe Mary wakiweka udongo kwenye kaburi la marehemu Bernard Membe wakati alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye ibada ya mazishi ya Marehemu Membe yaliyofanyika kijijini kwake, Rondo, Chiponda Mkoani Lindi. Mei 16, 2023 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na waombolezaji wakati alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye ibada ya mazishi ya Marehemu Bernard Membe yaliyofanyika kijijini kwake, Rondo, Chiponda Mkoani Lindi. Mei 16, 2023 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete wakati alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye ibada ya mazishi ya Marehemu Membe yaliyofanyika kijijini kwake, Rondo, Chiponda Mkoani Lindi, Mei 16, 2023 Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainab Telack (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*Asema atakumbukwa na Jumuiya za Kimataifa kwa utumishi wake
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaomba watanzania kumuombea na kuenzi yote mazuri aliyowahi kufanya marehemu Bernard Kamilius Membe enzi za uhai wake.
Amesema hayo leo Jumanne (Mei 16, 2023) alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia katika ibada ya mazishi ya Marehemu Bernard Membe iliyofanyika kijijini kwake Chiponda, Rondo Mkoani Lindi
“Watanzania, Wanalindi na hapa Rondo, Mheshimiwa Rais Samia amewataka muenzi yale yote mema aliyotenda wakati wa uhai wake, lakini pia endeleeni kumuombea ili mwenyezi Mungu amlaze mahali pema”
Waziri Mkuu amesema kuwa Rais Dkt Samia amesema kifo cha Bernard Membe kimewaacha watanzania na Wana-Lindi na butwaa kubwa, simanzi na huzuni, “Amesema anatoa pole sana kwa wote walioguswa na msiba huu ndani na nje ya nchi yetu”
Rais Samia amesema kuwa Marehemu Membe atakumbukwa kwa mengi na watanzania na jumuiya za kimataifa kutokana na utumishi wake uliotukuka katika nafasi mbalimbali alizohudumu wakati wa uhai wake
“Marehemu Membe atakumbukwa kwa usikivu wake, upole na weledi katika kufanya majukumu yake, uzalendo wa Taifa na mwenye msimamo thabiti, alikuwa mfano mzuri wa kuigwa”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wana-Rondo kumuezi Membe kwa kutunza yale yote aliyoyaanzisha na kuyasimamia katika eneo hilo.
Kwa upande wake Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Kikwete amesema kuwa Marehemu Bernard alikuwa Mwanadiplomasia mbobezi, Mwanamikakati makini na mchumi mzuri
Amesema kuwa katika kipindi cha Miaka tisa akiwa Waziri wa Mambo ya Nje alifanya kazi kubwa ya kuendeleza maslahi ya Tanzania katika medani za Kimataifa na kikanda”
Naye Mbunge wa Jimbo la Mtama na Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mheshimiwa Nape Nnauye amesema kuwa Membe alikuwa mwalimu wa wengi, mzalendo, jasiri na mwenye mapenzi makubwa kwa nchi “Sisi wanafunzi wake tutalinda, tutadumisha na kuendeleza kila aliloliweka na kuliwekeza kwetu”
Marehemu Bernard Membe ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa alifariki Mei 12, 2023 katika hospitali ya Kairuki Jijini Dar es Salaam