Featured Kitaifa

NAIBU KATIBU MKUU MKAMA AASA UADILIFU UKAGUZI WA MAZINGIRA

Written by mzalendoeditor

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Switbert Mkama amewaasa maafisa mazingira na wakaguzi wa migodi kuwa waadilifu ili kutimiza azma ya Serikali ya kupunguza matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu. 

Ametoa wito huo wakati akifungua warsha ya siku mbili kwa Maafisa Mazingira na Wakaguzi wa Migodi kuhusu Mikataba ya Minamata na Basel kwa ajili ya kupunguza matumizi ya Zebaki iliyoanza Mei 03, 2023 jijini Dodoma.

Dkt. Mkama amesema kuwa Tanzania ilisaini Mkataba wa Tanzania ilisaini Mkataba wa Minamata kuhusu zebaki Oktoba 10, 2013 kwa lengo la kupunguza matumizi ya kemikali hiyo yenye athari kwa afya na mazingira.

Amewaasa wakaguzi kuwa waadilifu katika shughuli zao kwani bila uadilifu kama nchi tutakwenda mbele hatua moja na kurudi nyuma katika kupunguza matumizi ya zebaki.

”Nawaomba muepuke kuchanganya maslahi binafsi na ukaguzi ili kuhakikisha afya na mazingira yanakuwa salama na tutambue zebaki ina athari kiafya na mazingira,” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Utunzaji wa Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usamamizi wa Mazingira (NEMC) Mhandisi Redempta Samuel amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo wa kutatua changamoto za kimazingira.

Amesema shughuli nyingi za uchimbaji mdogo wa dhahabu zinafanyika katika maeneo ya vyanzo vya maji na misitu na kuhusisha uharibifu wa mazingira hivyo warsha itawapa uelewa kukabiliana na changamoto hizo.

Naye Lucas Maselo kutoka Tume ya Taifa ya Madini amesema mafunzo yatawajengea uwezo wa kuanza kuchagiza matumizi ya teknolojia ya kisasa ya uchenjuaji wa dhahabu badala ya zebaki.

Amesema kuwa teknojia mpya pia itakuwa na manufaa kwa wachimbaji wadogo kwa kuwa mbali ya kulinda afya zao lakini pia itasaidia kuwaongezea kipato kwani wataongeza uzalushaji wa dhahabu.

 

About the author

mzalendoeditor