Featured Kitaifa

GUGU ARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI WA MIRADI YA MAENDELEO

Written by mzalendoeditor

Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Gugu akikagua ujenzi wa moja ya madarasa yaliyokamilika katika Shule ya Msingi Soya, Wilaya ya Chemba. Darasa hilo ni kati ya vyumba tisa vya madarasa, Jengo la Utawala na matundu 30 ya Vyoo ambavyo ujenzi wake uko katika hatua za mwisho. Ujenzi wa majengo hayo umegharimu kiasi cha shilingi milioni 250,000.

Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Gugu akikagua jengo la utawala ikiwa ni sehemu ya ujenzi wa Zahanati ya Mlongia, Wilaya ya Chemba. Zahanati ya Mlongia iko katika hatua za mwisho za ukamilishaji na kiasi cha Shilingi milioni 50 zimetolewa na Serikali katika kukamilisha ujenzi wake

Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Gugu akizungumza na watumishi wa Wilaya ya Chemba katika moja ya ziara zake za kukagua miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Dodoma.

Serikali Mkoani Dodoma imeendelea kuimarisha miundombinu katika sekta ya Elimu na Afya kwa lengo la kuboresha na kusogeza huduma kwa wananchi.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 02/05/2023 na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Gugu alipofanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Chemba kukagua miradi ya maendeleo.

Bw. Gugu ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa madarasa, maabara na zahanati katika Vijiji vya Jangalo, Soya na  Ombiri ambapo ujenzi wake uko katika hatua za mwisho na umegharimu kiasi cha Shilingi millioni 90.6 kwa madarasa 12 na maabara 1, kwa upande wa ujenzi wa zahanati umegharimu kiasi cha Shilingi millioni 50.

“Ndugu zangu Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya kukamilisha miradi hii ya maendeleo, nitoe rai kwenu kwanza kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati, pili miradi ikamilike kwa ubora wa hali ya juu” Gugu amesisitiza.

Nae Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba Bi. Siwema Jumaa amesema mbali ya fedha kutoka Serikali kuu utekelezaji wa miradi hiyo ni pamoja na jitihada za nguvu za wananchi ambao kwa baadhi ya majengo ya zahanati na madarasa wananchi wamejenga maboma.

Pia, amewataka wakazi wa vijiji vya Jangalo ,Soya na Ombiri kuwa walinzi namba moja wa miradi hiyo kwa kuwa inaghariimu fedha nyingi za Serikali.

Ziara ya Bw. Gugu ilianzia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wa Chemba na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Chemba kuongea na watumishi na kufanikiwa kukagua umaliziaji wa vyumba vitatu vya madarasa shule ya Msingi Ombiri, ujenzi wa vyumba tisa vya madarasa, jengo la Utawala, matundu 30 ya vyoo katika shule ya Msingi Soya, umaliziaji wa chumba 01 cha maabara shule ya Sekondari Jangaro na ujenzi wa Zahanati ya Mlongia.

Katika hatua nyingine Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Senga Gugu amefanikiwa kuongea na  watumishi na  kuwaasa  kufanya kazi kwa weledi, ushirikiano, kupendana na kufanya kazi kwa ubora na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea .

About the author

mzalendoeditor