Featured Kitaifa

WANANCHI WA KUSINI WAELEZEA WANAVYONUFAIKA NA MRADI WA REGROW

Written by mzalendoeditor

Wakazi wa Kijiji cha Tungamalenga mkoani Iringa wameendelea kutoa shukrani zao kwa Serikali kupitia Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) jinsi unavyosaidia Wananchi wanaoishi pembezoni mwa Hifadhi za Kipaumbele kwa kutoa ufadhili wa masomo wa vyuo mbalimbali hapa nchini .

Wakizungumza wananchi hao leo katika Kijiji cha Tungamalenga kwa nyakati tofauti wamesema Mradi huo umewanufaisha wananchi hao kiuchumi na kielimu kwa ustawi wa watoto wao.

Anjelika Kasimba, ambaye ni Mnufaika wa Mradi wa REGROW amesema REGROW ni miongoni mwa mradi bora ambao mara baada ya kukamilika kwake utaacha alama isiyofutika kwani anaamini Mtoto wake aliyepata ufadhili wa masomo katika Chuo cha Mafunzo ya Wanyamapori Pasiansi mara baada ya kuhitimu masomo yake atajikwamua kiuchumi yeye pamoja na familia yake .

Ameongeza kuwa mbali ya ufadhili huo wa masomo kwa mtoto wake, Mradi huo pia umemtoa kimasomaso kwa kumuwezesha kupata fedha mbegu ambazo zimemsaidia kujiinua kichumi kwa kulima eneo kubwa ambapo anategemea kupata mavuno mengi kwa mwaka huu.

Ameongeza kwamba tokea Mradi huo uanze kugusa maisha ya wananchi wa Tungamalenga yeye pamoja na Wanawake wenzake wamepata hamasa ya kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kurejesha marejesho na pia kuwa Wanufaika wa miradi mbalimbali ya kiuchumi ikiwemo COCOBA na ufugaji nyuki.

Devota Mgesi mwananchi wa Tungamalenga ameipongeza serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha Mradi huo unatoa fedha za kutosha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ufugaji nyuki katika Kijiji hicho na kusema kuwa ufugaji huo wa nyuki utawaongezea kipato maradufu kwa siku za usoni.

“Kwa hiki kinachofanyika sasa tuna kila sababu ya kujivunia Mradi huu wa REGEROW, kwani kupitia mradi huu watoto wetu wanasomeshwa Vyuo vikuu tunataka miradi mingine ya namna hii ambayo inawagusa watoto wa kimaskini kwani nina uhakika kabisa bila mradi huu mtoto wangu asingekwenda Chuo cha Wanyamapori Mweka” amesema

Aneth Kyaulilo ambaye ni Mwezeshaji Jamii wa Mradi wa Regrow amesema Mradi huo umeboresha maisha ya wananchi ambapo katika Kijiji cha Tungamalenga hadi sasa kuna vikundi saba ambavyo vimepewa Mil.48 kwa ajili ya kujiendeleza kiuchumi kupitia Mradi wa REGROW

Ameeleza kuwa Mradi huo wa REGROW umekuwa msaada mkubwa kwa wananchi na mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa na hii imesaidia vikundi mara baada ya kuundwa vimekuwa vikipewa mafunzo namna ya kuanzisha miradi ya kimkakati kiuchumi

Naye, Fedrick Funzila ambaye ni Mwenyekiti wa kijiji hicho amesema anajivunia Mradi wa REGROW kwani umekuwa neema kwa wananchi wake na umewapanua kimawazo namna ya kuchangamkia fursa za kiuchumi.

Kwa upande wake Mratibu wa Regrow, Dkt. Aenea Saanya amesema moja ya vigezo vya utekelezaji wa Mradi huo ni kuhakikisha Wananchi wanakuwa wanufaika namba moja katika maeneo yote ambapo Mradi huo unapotekelezwa.

Mradi wa REGROW ulianzishwa mwaka 2017 kwa lengo la kupanua wigo wa mazao ya utalii kijiografia kwa kuendeleza Sekta ya Utalii katika Mikoa ya Kusini. Mradi huo unatekelezwa kupitia fedha za mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Marekani Milioni 150 kutoka Benki ya Dunia

About the author

mzalendoeditor