Featured Kitaifa

MRADI WA HEET KUSAIDIA KUBORESHA MITAALA SUA.

Written by mzalendoeditor
 
Na Farida Mangube. Morogoro 
Katika kuwasaidia vijana wanaomaliza masomo ya Chuo Kikuu kupata ajira, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimefanya Warsha ya Maboresho ya Mitaala yanayoendana na Matakwa ya Soko la Ajira ambayo ni sehemu ya Mradi wa Kuendeleza Vyuo Vikuu ili kuleta Mageuzi  Kiuchumi Tanzania 
 Warsha hiyo ya siku tatu inayofanyika katika Kampasi ya Edward Moringe imewakutanisha Wakuza Mitaala kutoka Idara mbalimbali za Kitaaluma SUA, Wawakilishi toka Wizara ya Elimu,  Benki ya Dunia pamoja na Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu Tanzania TCU.
Akizungumza nje ya warsha hiyo Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo upande wa  Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala amesema maboreaho hayo yatajikita zaidi katika maswala ya stadi za kazi, soko la ajira pamoja na wanafunzi wanaohitimu kuweza kuajirika na kujiajiri.
Amesema kwa sasa zoezi lililopo ni kupitia Mitaala yote iliyopo  chuoni hapo ambapo kuna ambayo itafutwa kwa sababu imepitwa na wakati, kufanyiwa marekebisho na ile ambayo itaunganishwa ili kuendana na wakati pamoja na kuja na Mitaala mipya.
“Kutokana na Mabadiliko ya Teknolojia tunataka Mitaala ambayo itakuwa imesheheni Teknolojia za kisasa ndio maana tunaenda mbele ili tuingie katika ulimwengu wa Uchumi wa Viwanda na Mapinduzi ya Viwanda ambayo yatatawaliwa zaidi na Teknolojia”. Alisema Prof. Mwatawala.
Aidha kwa upande wake Dkt. Jamal Jumanne Athuman ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uratibu wa Uboreshaji na Ukuzaji wa Mitaala SUA amesema warsha hiyo ya siku tatu inalenga kuwajengea uwezo wakuza Mitaala SUA ili waweze kutengeneza Mitaala ambayo inakwenda na mahitaji ya wakati na kutoa ujuzi ambao unatakiwa ili kukuza uchumi. 
Amesema wanahitaji Mitaala ambayo kwanza ina Maudhui ya kisasa lakini pia ambayo inajenga umahiri, inakubalika kimataifa, inatoa fursa za kujenga Ubunifu pamoja na kutengeneza mahusiano na soko la ajira kwa kuwa kuna uhusiano mkubwa sana kati ya aina ya elimu inayotolewa na ukuaji wa Uchumi.
” Warsha hii inaenda kuwapatia uwezo wakuza mitaala na kuwakumbusha majukumu yao kama wakuza Mitaala ambapo kupitia mafunzo watakayopata wataweza kujifunza na kutambua mahitaji ya Soko la Ajira na kuandaa Mitaala inayotayarisha wahitimu kwa ajili ya soko hilo”,amesema Dkt. Jamal Jumanne.
Naye Dkt. Agnes Sirima Kaimu Rasi Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii ambaye ni miogoni mwa washiriki katika Warsha hiyo amesema wanaishukuru Benki ya Dunia kupitia Mradi wa HEET pamoja na Menejimenti ya Chuo kwa kuwaandalia mafunzo ambayo yataenda kuwasaidia kugundua namna bora ya kutengeneza Mitaala ambayo itakidhi soko la ajira na kuweza kusaidia katika kuboresha uchumi.

About the author

mzalendoeditor