OR – TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Angellah Kairuki amekabidhi magari 25 ikiwa ni sehemu ya Magari 200 yaliyoagizwa kupitia mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) kwa ajili ya Maafisa Elimu Sekondari wa Halmashauri zote nchini.
Pia ameahidi kujenga bweni la wanafunzi wa kiume wa shule ya sekondari Kibasila ikiwa ni ahadi kutoka kwa Mheshimiwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza mkoani Dar es Salaam katika hafla ya ugawaji wa magari hayo Mhe. Kairuki
aliwataka Wakala wa Ununuzi Serikalini (GPSA) kukakamilisha upatikanaji wa magari mengine 105 yaliyosalia kwa ajili ya mafisa elimu hao.
“Katika Halmashauri 184 zinazotakiwa kupata magari, Halmashauri 51 tayari zimepata katika awamu ya kwanza, awamu ya pili 19 na hii awamu ya tatu magari 25 hivyo bado magari 105 kwa maofisa hayo,” alisema.
Aidha, ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha elimu na maslahi ya walimu nchini hivyo aliwataka maofisa hao wawe wabunifu kusimamia shughuli za Kielimu na kuhakikisha kuwa Ubora wa Elimu unaimarika.
Mhe. Kairuki amesema elimu ya sekondari inahitaji uwajibikaji na huwezi kupata mafanikio pasipo kuwa na ubunifu na bidii kwa watumishi hivyo Serikali inaendelea kufanya maboresho lakini pia wasimamizi nao watekeleze wajibu wao.
Amewataka Maafisa hayo kutumia magari hayo kuongeza ufanisi wa shughuli za Kielimu na pia yatunzwe ili yaweze kudumu kwa muda mrefu.
Vilevile aliwataka wanafunzi waliohudhuria hafla hiyo kukazania masomo na kuepuka kuingia kwenye tabia zinazopingana na Mila na desturi za nchi.
Aliwataka wafuate mambo mazuri ya kizalendo yanayofundishwa na wazazi na walimu ili kukuza kiwango cha ufaulu.
“Akizungumzia kuhusu ujenzi wa bweni la watoto wa kiume kwenye shule ya Kibasila amesema ni ahadi kutoka kwa Rais Dk.Samia kwa sababu alitaka kujua hitaji la shule hiyo na kutuelekeza sisi wasaidizi wake tulitatue na hivyo tunatekeleza agiza la Mhe. Rais.
Naye Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Abdul Maulid aliishukuru TAMISEMI kwa kutoa magari hayo kwani yamekuwa yakiwasaidia katika Ufuatiliaji wa elimu.
Pia aliipongeza serikali kwa kuwasikiliza na hivyo kwa niaba ya maofisa elimu wote ameahidi kulipa fadhila ya magari hayo kwa kutenda haki kwa kuwafuata walimu walipo.