Featured Kitaifa

VIJANA WAISHUKURU SERIKALI URATIBU IMARA WA AJIRA NJE YA NCHI

Written by mzalendoeditor
Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Joseph Nganga akizungumza na Vijana waliopata fursa za ajira nchi ya Saudi Arabia wakati wa zoezi la kuwaaga vijana 50 uwanja wa ndege wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam
Sehemu ya Vijana wanufaika wa ajira nchi ya Saudi Arabia wakisikiliza maelezo ya Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Ajira Bw. Joseph Nganga wakati wa zoezi la kuwaaga vijana 50 lililofanyika katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam
Kijana Mnufaika wa Ajira nje ya nchi, Samir Issa akitoa neno la shukrani kwa serikali wakati wa zoezi la kuwaaga vijana 50 kuelekea Saudi Arabia, katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Kampuni ya wakala wa ajira Bravo Job Center Agency, Bw. Abbas Mtemvu akieleza jambo wakati wa tukio hilo.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Joseph Nganga (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na watendaji wa Bravo Job Center Agency na Vijana waliopata fursa za ajira nchi ya Saudi Arabia mara baada ya kuwaaga katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam tarehe 17 Aprili, 2023.

PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU

(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)

Na: OWM – KVAU – DAR ES SALAAM
Vijana waliopata fursa za ajira nje ya nchi wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuja na njia bora za kuratibu na kusimamia watu wanaoajiriwa nje ya nchi kwa lengo la kulinda haki za watanzania.
Pongezi hizo zimetolewa Aprili 17, 2023 wakati wa zoezi la kuwaaga vijana 50 ambao wamepata fursa za ajira nchini Saudi Arabia kupitia Kitengo cha Huduma za Ajira (TaESA) kwa kushirikiana na kampuni ya wakala wa ajira Bravo Job Center Agency. 
Akizungumza mmoja wa wanufaika, Exaver Jauri amesema kumekuwa na dhana potofu hususan zinapotokea fursa za ajira nje ya nchi na kuwashauri vijana kuacha kuwa na mitazamo potofu kwa kuwa serikali kupitia TaESA imekuwa ikiratibu na kusimamia ajira za watanzania nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Ajira Bw. Joseph Nganga amesema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia TaESA imeendelea kuwaunganisha watafuta kazi na waajiri ndani na nje ya nchi pamoja na kusimamia michakato yote ya watu wanaoenda kufanya kazi nje ya nchi.
“Katika kuratibu ajira za watanzania wanaoenda kufanya kazi nje ya nchi, TaESA imekuwa ikishirikiana kwa karibu na balozi zetu kwa lengo la kuthibitisha uhalisia wa kazi zinazotolewa ili kuhakikisha kazi wanazoenda kufanya ni za staha,” amesema
Ameongeza kuwa Serikali imeingia kwenye makubaliano na baadhi ya nchi ili kuwa na mikataba kati ya nchi itakayojenga misingi mizuri ya ufanyaji kazi sambamba na kuongeza fursa za ajira kwa watanzania wengi zaidi kuajiriwa nje ya nchi. 
Aidha, amewasihi vijana hao kuzingatia bidii katika kazi, kuwa waadilifu, wabinifu, kujenga mtazamo chanya wa ajira wanazofanya pamoja na kufuata taratibu sahihi za mawasiliano katika maeneo ya kazi.
“Watanzania tunasifika ulimwenguni kwa maadili mema, natarajia mtaenda kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia misingi ya maadili yetu,”amesema.
Naye, Mwenyekiti wa Kampuni ya wakala wa ajira Bravo Job Center Agency, Bw. Abbas Mtemvu amewataka vijana kujitokeza kwa wingi zaidi na kujiandikisha TaESA ili fursa hizo zitakapotangazwa kwa mara nyingine waweze kunufaika. 

About the author

mzalendoeditor