Featured Kitaifa

UTUMISHI WA UMMA USICHANGANYWE NA SIASA – MHE. OTHMAN

Written by mzalendoeditor

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman amesema Nchi hii imeanzia mbali katika Mfumo Rasmi wa Utumishi wa Umma wa kujivunia, ambao unahitaji kulindwa na kuenziwa, ili kujenga ufanisi na maendeleo.

Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo akifungua Mafunzo juu ya Maadili ya Utumishi wa Umma na Usalama Kazini, kwa Watendaji na Wafanyakazi wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, hapo katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil, Kikwajuni Mkoa wa Mjini-Magharibi, Unguja.

Amesema, hiyo ni kutokana na ukweli kwamba Mfumo wa Utumishi wa Umma Nchini, ambao umepita katika Vipindi muhimu tofauti, uliasisiwa tangu na tangu, katika zama ambazo Mataifa Mengi, kuanzia Kusini mwa Jangwa la Sahara na hata Afrika yote, hawakuwa nao.

Amebainisha Mwaka 1890 kuwa ndipo ulipoasisiwa Mfumo huo kupitia kile kilichoitwa ‘Departmental System, kabla ya kupita Marekebisho, katika Awamu za 1906, 1924, 1960, 1965, na hatimaye kufikia kuja kwa Katiba ya Awali mnamo Mwaka 1979, na kisha Katiba ya Sasa ya 1984.

Mheshimiwa Othman amefahamisha kwa kusema, “wapo ambao wanapenda turudi katika Mfumo ule wa Kimapinduzi lakini ni vyema kuzingatia kwamba kila jambo lina wakati wake, kwa mujibu wa Kanuni, Miongozo na Sheria”.

“Licha ya kuwepo Mfumo huo, suala ni jee kwa kiasi gani misingi ya maadili ya utumishi wa umma na usalama kazini imetekelezwa’, ameeleza na kuhoji Mheshimiwa Othman.

Mheshimiwa Othman amebainisha baadhi ya mambo ambayo yamekuwa ni chanzo cha kudhoofika kwa Mfumo wa Utumishi wa Umma wenye ufanisi, yakiwemo ya ukosefu wa ‘meritocracy’ na uajiri unaojali vigezo.

Akifafanua mambo hayo, Mheshimiwa Othman amesema kuwa uajiri usiozingatia vigezo; wenye upendeleo, na upambe wa kisiasa, kwa namna fulani umeporomosha Mfumo wa Utumishi wa Umma Nchini, na kwamba “mchongoma hauwezi kuzaa zabibu”.

Aidha ametoa wito kwa Viongozi, Watendaji na Watumishi wa Umma, pamoja na kila mmoja kuheshimu pahala sahihi pa kuiweka elimu na taaluma yake, kuzingatia nguvu ya maadili, ili kujenga ufanisi katika jamii, Nchi na Taifa kwa ujumla.

Akiongelea juu ya Usalama Kazini, Mheshimiwa Othman amewataka Viongozi kuzingatia Miongozo, Kanuni, pamoja na Kuangalia Mazingira Yaliyosalama Pahala pa Kazi, ili kujenga Ufanisi.

Kwa upande wake , Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Mhe. Harusi Said Suleiman, amesema Semina hiyo Elekezi ni katika fursa muhimu kwa Watendaji na Wafanyakazi Nchini, ili kujenga ufanisi katika kuutumikia Umma.

Naye, Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dokta Omar Dadi Shajak, ameeleza kwamba lengo la Semina hiyo ni kutekeleza kwa Vitendo, Agizo la Mheshimiwa Rais wa Zanzibar, Dr. Hussein Ali Mwinyi, kwamba Watendaji na Wafanyakazi wote hapa Visiwani, wapate Mafunzo juu ya Haki, Wajibu na Usalama Wao, katika Utumishi wa Umma na Pahala pa Kazi.

Mafunzo hayo ambayo ni ya Siku Mbili, kwa Unguja na Pemba, yamewajumuisha Wafanyakazi na Watendaji wote wa Idara na Taasisi ziliopo chini ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais zikiwemo Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu; Tume ya UKIMWI; Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira; na Mamlaka ya Udhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.

Kumekuwepo na Uwasilishaji wa Mada mbali mbali za Mafunzo hayo, zikiwemo za Maadili ya Watumishi wa Umma; na Usalama na Afya Kazini, ambazo zimewasilishwa na Nd. Maulid Shaib Ahmada na Bw. Ame Faki, kutoka Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, ambao kwa ujumla wamesisitiza umuhimu wa kuzingatia taaluma, heshima, nidhamu, haki na usawa bila upendeleo katika utoaji wa huduma.

About the author

mzalendoeditor