MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amechangia mjadala wa hotuba ya Waziri Mkuu ya 2023/2024,na kutoa ombi la kubadili majina ya majimbo ya Singida Mashariki na Singida Magharibi ili kuweka jina lenye utambulisho wa eneo husika.
Akichangia mjadala huo April 13,2023,bungeni Jijini Dodoma Mtaturu amesema tayari kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa (RCC),ya Singida.
“Sisi wilaya ya Ikungi tuna majimbo mawili yakiutawala lakini majimbo hayo yamepewa majina ambayo hata mtu akiangalia haraka haraka hajui jimbo lipo wapi ,sisi hatuombi eneo jipya tunaomba jina libadilike ,
“Tunayo Singida Mashariki na Singida Magharibi,mfano tukipewa jina la Jimbo la Ikungi badala ya Singida Mashariki angalu inaweza leta maana nzuri au ukiletewa jimbo la Puma au Sepuka badala ya Singida Magharibi walau utakuwa umeweka utambulisho wa eneo husika,naamini jambo hili sio kubwa na pacha wangu Kingu amepiga makofi ina maana anakubaliana nami,”amesema.
Amesema dhamira ya kufanya hivyo ni kuhakikisha kwamba wanapata utambulisho halisi ya majimbo hayo na wananchi wajue wabunge wao wanapotaja majina ya majimbo yenye utambulisho wajue wanatoka wilaya ya Ikungi.
MAJIBU YA SERIKALI .
Akijibu ombi hilo ,Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Bunge na Uratibu Jenista Mhagama amesema wamepokea ombi hilo.
“Tumepokea ombi la mbunge Mtaturu ameomba hapa kuangalia majina ya majimbo katika eneo analotoka,sasa ibara ya 74 kifungu kidogo cha 6 (c) na ibara ya 75 imeipa jukumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),kuratibu,kutathimini na kujenga mipaka ya majimbo nchini,
“Kutokana hilo tunaomba muda utakapofika Mtaturu na Kingu pelekeni mapendekezo ya majina hayo,na hasa kama hayatakuwa na gharama ya kuyagawa na kuyapanga upya basi tutaangalia jina litakalolingana na sifa na stahiki na matakwa ya wananchi,”amesema.