Featured Kitaifa

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA MKUTANO WA MAJAJI JIJINI MWANZA

Written by mzalendoeditor

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akihutubia Majaji pamoja na watumishi wa Mahakama wakati akifungua Mkutano wa Majaji wa Tathimini ya Utendaji wa Mahakama na kufanya Mapitio ya Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021 – 2024/2025 leo tarehe 12 Aprili 2023 katika Ukumbi wa Malaika mkoani Mwanza.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Prof. Ibrahim Juma wakati alipowasili katika Ukumbi wa Malaika Jijini Mwanza kufungua Mkutano wa Majaji wa Tathimini ya Utendaji wa Mahakama na kufanya Mapitio ya Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021 – 2024/2025

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Prof. Ibrahim Juma, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Pauline Gekul katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama ya Rufani mara baada ya kufungua Mkutano wa Majaji wa Tathimini ya Utendaji wa Mahakama na kufanya Mapitio ya Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021 – 2024/2025 leo tarehe 12 Aprili 2023 katika Ukumbi wa Malaika mkoani Mwanza.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Mhimili wa Mahakama kushiriki kikamilifu katika kazi ya kufanya tathmini ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2025 pamoja na maandalizi ya Dira mpya ya Maendeleo 2050 ili kuenda sambamba na mfumo wa sheria na utawala bora unaohitajika utakaolingana na mikakati ya kiuchumi.

Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 12 Aprili 2023 wakati akifungua Mkutano wa Majaji wa Tathimini ya Utendaji wa Mahakama na kufanya Mapitio ya Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021 – 2024/2025 unaofanyika katika Ukumbi wa Malaika mkoani Mwanza. Amesema katika kipindi cha miaka 25 ijayo Tanzania inatarajiwa kutumia rasimali zake, fursa mbalimbali, teknolojia na ubia wa kimkakati katika kupiga hatua kubwa zaidi ya maendeleo na kufikia uchumi wa kipato cha juu hivyo Mhimili wa Mahakama unapaswa kutoa kipaumbele kushiriki ipasavyo katika zoezi hilo muhimu kwa mustakabali wa Taifa.

Halikadhalika Makamu wa Rais ametoa rai kwa Mahakama kuzingatia ufanisi wa shughuli za utoaji haki nchini kwa kutambua kwamba ni nguzo muhimu ya kulinda amani na utulivu katika nchi lakini pia kukuza utawala wa sheria pamoja na shughuli za kiuchumi, biashara na uwekezaji. Amewasisitiza Majaji, Mahakimu, na watumishi wote wa Mahakama kutumia Mkutano huo kujadili na kutathmini masuala muhimu yanayoathiri utendaji wao na kuandaa mapendekezo yenye tija ambayo yataongeza ufanisi na kuboresha mfumo wa utoaji haki nchini. 

Makamu wa Rais Dkt. Mpango ametoa wito wa kufanyia kazi masuala mbalimbali katika mfumo wa utoaji haki ikiwemo kusogeza huduma za Mahakama za Mwanzo karibu na wananchi, kufanya maboresho yatakayopelekea kupunguza urasimu ili kuharakisha kukamilika kwa mashauri na kuhakikisha wanaoshinda kesi za madai wanapata haki zao, kuendelea kuboresha matumizi ya tehama pamoja na kutumia Mkutano huo kufanya tathmini ya mianya na viashiria vya rushwa na kuchukua hatua stahiki.

Aidha Makamu wa Rais ameongeza kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ina dhamira ya dhati ya kuboresha utendaji wa Mahakama ili kuiwezesha kutoa haki kwa wananchi na ustawi wa Taifa. 

Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Prof. Ibrahim Juma ametoa wito kwa wananchi kufuata taratibu katika njia za utafutaji haki kisheria kabla ya kufikisha malalamiko kwa viongozi wa serikali. Amesema zipo njia sahihi ikiwemo kutoa taarifa kwa taasisi zinazosimamia maadili pale mwananchi anapoona hajatendewa haki na ukiukwaji wa maadili umefanyika.

Prof. Juma amesema Mkutano huo ni nafasi kwa watumishi wa mahakama na wadau mbalimbali kwa kuwa tathimini inayofanyika inagusa sekta zote za uchumi, siasa pamoja na huduma. Aidha ameongeza kwamba mkutano huo ni fursa kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani kwa kuwa watapata nafasi ya kufahamu maboresho mbalimbali ili kuzingatia kwamba majalada wanayoamua yanahusu maisha ya watu na uchumi.  

About the author

mzalendoeditor