MDHIBITI na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere,akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 6,2023 jijini Dodoma mara baada ya kukabidhi ripoti yake ya ukaguzi wa hesabu za serikali ya mwaka 2021/2022 bungeni Dodoma.
SEHEMU ya Waandishi wa habari wakimsikiliza Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere (hayupo pichani) wakati akizungumza mara baada ya kukabidhi ripoti yake ya ukaguzi wa hesabu za serikali ya mwaka 2021/2022 bungeni Dodoma leo Aprili 6,2023 jijini Dodoma
Na.Alex Sonna-DODOMA
MDHIBITI na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere amesema ripoti yake ya ukaguzi wa hesabu za serikali ya mwaka 2021/2022 imebaini kuwepo kwa mashirika ya umma kujiendesha kwa hasara kwa miaka miwili mfululizo .
CAG Kichere ameyasema hayo leo Aprili 6,2023 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukabidhi ripoti hiyo bungeni jijini Dodoma.
Amesema kuwa katika fedha za Uviko-19 ripoti hiyo imebainisha madudu kadhaa, ikiwemo bidhaa zenye thamani ya zaidi ya Sh50 bilioni zilizolipiwa fedha hazijapokewa.
”Septemba 7, 2021 Tanzania ilipokea mkopo wenye masharti nafuu wa Dola 567.25 milioni (sawa na Sh 1.29 trilioni) kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) ambazo zilielekezwa sekta za afya, elimu, maji na utalii na mazingira.”amesema CAG Kichere
Aidha amesema kuwa mbali na sekta hizo, sehemu ya fedha hizo ilipelekwa katika sekta za ulinzi wa jamii, nishati, uwezeshaji uchumi, uratibu na usimamizi ambapo Tanzania Bara ilitumia Sh1 trilioni na Zanzibar Sh230.1 bilioni.
”Uchunguzi mwingine ulibaini kuwa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) lilikuwa na madeni ya Sh21 bilioni ambayo uongozi haukuweza kutambua wadaiwa husika.Hayo yamebainishwa na CAG kupitia ripoti yake ya Mashirika ya Umma ya mwaka 2021/2022 iliyotolewa leo Alhamisi Aprili 6, 2023.”amesema
Pamoja na hayo CAG ameeleza kuwa katika ripoti hiyo kuwa katika kiasi hicho, Shirika la Mawasiliano Tanzania lilitoa mapendekezo kwa Bodi ya Shirika kufuta deni la Sh7.51 bilioni.
Pia amesema katika ripoti hiyo amebaini kuwepo kwa dawa zilizoisha muda wa matumizi ambazo zimehifadhiwa kwenye hospitali za rufaa jambo ambalo ni hatari endapo zikiingia kwenye mikono ya watu wasiokuwa waaminifu.
”Tumebaini hasara iliyotokana na muda wa matumizi ya dawa na bidhaa za afya kuisha kwa muda wake na hivyo kusababisha hasara ya Shilingi Bilioni 3.5.”amesema CAG
Kichere amesema kuwa katika ukaguzi , Ofisi yake imebaini Idara ya Jeshi la Magereza ina wahamiaji 4,419 haramu kutoka nchi mbalimbali, huku 1,264 wakiendelea kutumikia vifungo, 45 wamewekwa mahabusu na 3,110 wanaotakiwa kurejeshwa makwao.
Kichere ameongeza kuwa gharama za kuwahudumia wahamiaji hao ni kubwa, huku Chakula cha
mfungwa mmoja kilitengewa bajeti ya Sh. 5,000 kwa siku.
” Kitendo cha kuwa na wahamiaji 3,110 katika magereza hayo huigharimu Sh. bilioni 5.68 kwa
mwaka; hivyo kuipa mzigo serikali,”amesema Kichere
Amesema kuwa Idara ya Jeshi la Magereza imeitaka Idara ya Uhamiaji kuchukua hatua
stahiki za kuwarejesha makwao wahamiaji haramu wanaomaliza vifungo vyao ili kuepuka gharama za ziada. Waziri wa Mambo ya Ndani ametoa maagizo ya kuzuiliwa ili kuwabakisha wafungwa wa kigeni wanaohitaji kurejeshwa makwao. Hata hivyo, kuwafukuza wahamiaji haramu ni suala la
kidiplomasia linalohitaji mashauriano na Mabalozi wa nje ya nchi.
“Natoa wito kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ikishirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kufanya juhudi zaidi kuhakikisha kwamba maagizo yanatolewa kikamilifu ili kuwarejesha raia wa kigeni walioachiliwa huru nchini kwao na kutatua suala hili kwa ukamilifu wake, na hivyo kupunguza gharama zisizo za lazima,”amesema Kichere
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya hesabu za Serikali (PAC)Naghenjwa Kaboyoka amesema kuwa Kamati yake itachambua ripoti yote na kuwahoji washukiwa Kwa kutumia ushahidi .
“Kazi kubwa ya Kamati yetu ni kupeleka mapendekezo kwenye Bunge,Kamati hii ni jicho la Bunge Kwa kuangalia hesabu za Serikali na mashirika yake tukisha peleka mapendekezo ni kazi ya Bunge kuchukua hatua na watakao bainika wachukuliwe hatua,”amesema Mhe.Kaboyoka
Naye Mwenyekiti wa kamati ya hesabu za Serikali za mitaa (LAAC) Mhe.Halima Mdee amebainisha kuwa Kutokana na ripoti hiyo kutolewa wanajipanga kufanya mahojiano na wahusika na kupeleka mapendekezo Bungeni .
“Hii inashangaza, matatizo mengi yamekuwa sugu, tunashuhudia mengi ya madudu yamejirudia kwa miaka miwili,Hali hii inamaanisha hata hao wanaosimamia fedha za Umma nao ni sugu,”ameeleza Mhe. Mdee.