Featured Kitaifa

WATALII WA NDANI WAONGEZEKA KWA ASILIMIA 199-MAJALIWA

Written by mzalendoeditor

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya 2023/2024, bungeni  jijini Dodoma, Aprili 5, 2023.  Wengine kutoka kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Wziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Patrobas Katambi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema idadi ya watalii wa ndani imeongezeka kutoka watalii 788,933 mwaka 2021 hadi watalii milioni 2.4 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 199.5.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeendelea kuwa hifadhi bora duniani ambapo kwa miaka minne mfululizo kuanzia mwaka 2019 hadi 2022 imepata tuzo ya dhahabu ya utoaji wa huduma bora iliyotolewa na European Society for Quality Research.

Ameyasema hayo leo (Jumatano, Aprili 5, 2023) wakati akiwasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024 bungeni jijini Dodoma.

 

Amesema Serikali imeendelea kuimarisha sekta za maliasili na utalii kupitia utekelezaji wa programu mbalimbali ili kukuza utalii, kuitangaza nchi yetu na vivutio vyake kitaifa na kimataifa pamoja na kuimarisha mchango wa sekta hizo kwenye pato la Taifa.

Amesema katika mwaka 2022/2023, programu mbalimbali zimeendelea kutekelezwa ikiwemo Programu ya Tanzania – The Royal Tour na utangazaji wa vivutio vya utalii kupitia matukio mbalimbali na vyombo vya habari ikiwemo Tanzania Safari Channel.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kutokana na jitihada hizo, idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kutoka watalii 922,692 katika mwaka 2021 hadi kufikia watalii takriban milioni 1.4 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 57.7.

Waziri Mkuu amesema katika mwaka 2023/2024 Serikali itaendelea kuibua na kuendeleza mazao ya utalii ya kimkakati ikiwemo utalii wa fukwe, mikutano na matukio, meli, michezo na utamaduni.

Vievile, itaendelea kuimarisha miundombinu katika maeneo ya hifadhi, kukarabati majenzi ya kale na kuyatangaza kidijitali pamoja na kutekeleza mikakati ya kuongeza thamani ya mazao ya misitu.

About the author

mzalendoeditor