Featured Kitaifa

WAUMINI 702 KANISA LA WAADVENTISTA WASABATO WAFIKIWA NA ELIMU YA MARBURG .

Written by mzalendoeditor

Na.Elimu ya Afya kwa Umma.

Katika jitihada za Wizara ya Afya , Idara ya Kinga,Elimu ya Afya kwa Umma kwa kushirikiana na kamati za afya za Halmashauri,Mkoa wa Kagera na Wadau mbalimbali za kuhakikisha elimu ya Ugonjwa wa Marburg unafika kila kona na sehemu za ibaada mkoani Kagera, jumla ya wananchi 1139 na elimu hiyo katika kata za Miembeni na Kashai ikiwa ni pamoja na waumini 702 wa Kanisa la Waadventista Wasabato Bukoba mjini na Mafumbo .

Akizubgumza mara baada ya kutembelea katika makanisa ya Waadventista Wasabato Bukoba Mjini Kata ya Miembeni pamoja na Mafumbo Kata ya Kashai yaliyopo katika Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera, Mtaalam wa Afya kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu Manispaa ya Bukoba NeliaPeace Kaimukilwa amesema kwa kuwa serikali imeweka nguvu utoaji wa elimu katika mikusanyiko mbalimbali ya watu, leo wametumia fursa hiyo kutoa elimu kwa kanisa la Waadventista Wasabato Bukoba Mjini pamoja na Mafumbo ambapo siku ya Jumamosi ni siku ya ibaada kwa kanisa hilo.

Ameendelea kufafanua kuwa pamekuwa na mwitikio mkubwa katika utoaji wa elimu hiyo ambapo Kanisa la Waadventista Wasabato Bukoba Mjini waumini 548 wamepatiwa elimu ya Marburg huku Kanisa la Mafumbo wakipatiwa elimu watu 154 na kufikia jumla ya waumini 702.

“Mwitikio umekuwa mkubwa kila muumini alitamani kuendelea kupata ufafanuzi licha ya kuwa tumeingia katikati ya ibaada na niwashukuru sana kwa kutupokea na kutukaribisha na kutupa nafasi na kila mmoja ameuliza swali na kupata ufafanuzi hivyo niipongeze Wizara ya afya kwa kuwezesha hili ni katika kuhakikisha kila mtanzania anapata elimu kuhusu ugonjwa wa Marburg”amesema.

Nao baadhi ya Wazee Viongozi wa Makanisa akiwemo Bebilas Mashauri kutoka Kanisa la Waadventista Wasabato Bukoba Mjini pamoja na Bernice Masejo Mkurugenzi wa Afya kanisani hapo wamesema Kanisa hilo limekuwa mstari wa mbele katika kufuata kanuni za afya hivyo elimu kuhusu Marburg itakuwa kichocheo cha kuongeza juhudi za kuelimisha wengine huku wakiipongeza Wizara ya Afya kwa kufika kila sehemu kutoa elimu hiyo.

Miongoni mwa maswali yaliyoulizwa katika zoezi la utoaji wa elimu ya Marburg katika Kanisa la Waadventista Wasabato Bukoba Mjini na Mafumbo ni pamoja na hofu ya wananchi kutokana na kuvamiwa na tumbili katika makazi ya watu hasa katika mitaa ya Kahororo na watu wanawezaje kuwaepuka kama wanaweza kuambukiza, tofauti gani kati ya Marburg na Ebola huku mmoja wa Waumini akitoa ushauri kwa ulimwengu wa sasa kuachana kuishi kwa ulafi na kula visivyoliwa.

Pamoja na kutembelea Makanisa ya Kisabato siku ya ibaada ya Jumamosi ya leo April ,Mosi,2023, watalaam wa afya pia wametembelea katika maeneo mbalimbali kutoa elimu juu ya Marburg ikiwa ni pamoja na kituo cha bodaboda cha Mafumbo Society na kuelimisha watu 407 pamoja na soko dogo la Mafumbo na kufikia watu 30 na kufikisha jumla ya watu 1139.

Wakiwa katika kituo cha bodaboda cha Kahororo Zahanati senta ya Mafumbo Society baadhi ya hoja zilizoibuliwa ni pamoja na kundi la waendesha bodaboda kuliangalia upya katika mapambano ya Marburg ambapo mwendesha bodaboda aliyejulikana kwa jina la Elia Prician amesema suala la kofia ngumu(helment) kuchangia abiria linaweza kuchangia watu wengi kupitia jasho na unyevunyevu hivyo ameishauri serikali kusitisha uvaaji wa kofia ngumu kwa abiria.

About the author

mzalendoeditor