Featured Kitaifa

WAZIRI UMMY ATETA NA BALOZI WA MAREKANI

Written by mzalendoeditor

Na. WAF-Dodoma

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo amekutana na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Michael Battle kwenye ofisi za Wizara jijini Dodoma.

Katika mazungumzo yao Waziri Ummy amemwambia Balozi huyo kwamba Serikali ya Tanzania inawashukuru Marekani kwa kuendelea kushirikiana hususani kwenye maboresho katika sekta ya afya nchini.

Aidha, Waziri Ummy amesema Tanzania inafanya vizuri katika jitihada ya kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.

Amesema bado kuna changamoto ya ubora wa huduma na gharama za matibabu kwa wananchi hivyo Serikali inakuja na Bima ya Afya kwa Wote ili kuwaondolea adha ya matibabu wananchi wake.

Kwa upande wa watumishi Waziri Ummy amesema wana uhaba wa watoa huduma kwa asilimia hamsini na wanaendelea kuajiri watumishi kila mwaka.

Kwenye eneo la HIV amesema wanafanya vizuri katika eneo la 95-95-95 na Malaria na TB bado wanaendelea na mapambano dhidi ya magonjwa hayo

Naye, Balozi wa Marekani Dkt. Battle amesema kupitia CDC wataendelea kusaidia kuboresha afya za wananchi kupitia sekta ya afya na kutoa mafunzo kwa watoa huduma za afya ngazi ya jamii pamoja na wataalamu wa maabara katika uchunguzi wa magonjwa mbalimbali ikiwemo magonjwa ya milipuko.

Hata hivyo Balozi huyo amempongeza Waziri Ummy kwa kusimamia vizuri Wizara ya Afya hususan katika mapambano ya magonjwa ya mlipuko.

About the author

mzalendoeditor